Mitaguso Mikuu
1

MITAGUSO MIKUU

UTANGULIZI

Yesu Kristo aliwakabidhi mitume kumi na wawili uongozi wa Kanisa wakiwa kundi moja lenye mkuu
wake, yaani Petro. Vilevile waandamizi wao, yaani maaskofu wote, ni kundi moja na Papa wa Roma
ndiye mkuu wao. Huyo peke yake, na kundi la maaskofu likiwa pamoja naye na chini yake, ndio wenye
mamlaka ya juu katika Kanisa lote. Mamlaka hiyo inatumika kwa namna ya pekee unapofanyika
mtaguso mkuu, yaani mkutano maalumu wa maaskofu uliokubaliwa na Papa kuwa unawakilisha kundi
hilo lote. Hakuna uamuzi wa kudumu kuhusu ipi ni mikuu kati ya mitaguso yote iliyofanyika katika
historia ya Kanisa. Tangu karne XVI Wakatoliki wataalamu wa sheria za Kanisa wanatoa orodha yao,
ambayo kwa sasa ni kama ifuatavyo.

ORODHA YA MITAGUSO MIKUU

 Katika milenia ya kwanza ilifanyika mashariki (Uturuki wa leo):
1. Nisea I (mwaka 325)
2. Kostantinopoli I (381)
3. Efeso (431)
4. Kalsedonia (451)
5. Kostantinopoli II (553)
6. Kostantinopoli III (680-681)
7. Nisea II (787)
8. Kostantinopoli IV (869-870)
 Katika milenia ya pili ilifanyika magharibi (Italia, Ufaransa, Ujerumani, Uswisi na Vatikano ya leo):
9. Laterano I (1123)
10. Laterano II (1139)
11. Laterano III (1179)
12. Laterano IV (1215)
13. Lyon I (1245)
14. Lyon II (1274)
15. Vienne (1311-1312)
16. Konstanz (1414-1418)
17. Firenze (1431-1445)
18. Laterano V (1512-1517)
19. Trento (1545-1563)
20. Vatikano I (1869-1870)
21. Vatikano II (1962-1965)

HISTORIA YA MITAGUSO MIKUU

Mitaguso mikuu ya kwanza ilifanyika hasa ili kubainisha katika mafundisho yaliyogongana yapi
yanalingana na imani sahihi. Mwisho wake ulikuwa kutangaza dogma fulani na kutenga na Kanisa
watakaokataa kuiamini na watakaofundisha tofauti.
Mitaguso iliyofanyika baada ya farakano la mwaka 1054 kati ya Kanisa la mashariki na la
magharibi, pamoja na kulenga umoja uliovunjika na kufundisha dogma mpya, ilishughulikia zaidi
urekebisho wa Kanisa katika ngazi na nyanja zote. Kwa namna ya pekee Mtaguso II wa Vatikano tangu
uitishwe ulijulikana kuwa wa kichungaji, yaani usio na lengo la kufundisha dogma mpya wala kulaani
mafundisho mengine.

Mtaguso I wa Nisea (325)

Mtaguso I wa Nisea ndio mtaguso wa kwanza kuitwa (tangu mwaka 338) mtaguso wa kiekumeni,
yaani mtaguso wa dunia yote au mtaguso mkuu. Ndiyo sababu inashika nafasi ya pekee kati ya
mitaguso yote.
Uliitishwa na kusimamiwa na kaisari Konstantino Mkuu, aliyehofia mabishano kati ya raia wake
Wakristo kuhusu Yesu Kristo, ambayo yalihatarisha umoja na usalama wa Dola la Roma lililoanza
kuelekea kusambaratika. Yeye aliwaalika maaskofu wote wa dola, waliokuwa kama 1000 mashariki na
kama 800 magharibi. Washiriki walitokea hata nje ya dola hilo, kama vile Persia na Armenia.
Page 1 of 21


2
Katika hali hiyo mtaguso ulianza tarehe 20 Mei 325; washiriki walikuwa kama 318, wengi wao
wakitokea upande wa mashariki wa dola hilo. Upande wa magharibi uliwakilishwa na watu 4 kutoka
Ulaya na 1 kutoka Afrika. Papa Silvesta I (314-335) aliwakilishwa na mapadri wawili.
Asili ya mabishano ilitokea katika Kanisa la Aleksandria (Misri), ambapo kasisi Arios alikuwa
amekanusha umungu wa Yesu, na hivyo alihukumiwa na Sinodi ya Aleksandria ya mwaka 321,
iliyoitishwa na askofu Aleksanda wa Aleksandria. Hata hivyo Arios hakuacha mafundisho yake,
akakimbilia Palestina kwa rafiki yake Eusebio wa Nikomedia.
Basi, mtaguso ulikiri karibu kwa kauli moja kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu kwa maana
ana ousìa (yaani dhati) ileile ya Kimungu aliyonayo Baba. Ndiyo kiini cha Kanuni ya imani ya Nisea
iliyopitishwa na mtaguso.
Uamuzi mwingine wa mtaguso ulikuwa kupanga siku ya Pasaka, sherehe kuu ya Kanisa, iwe
Jumapili inayofuata mbalamwezi ya kwanza ya majira ya Springi, tofauti na kalenda ya Kiyahudi. Pia
zilitungwa kanuni 20 kuratibu mambo mbalimbali.
Mtaguso ulipomalizika tarehe 25 Julai 325, Konstantino alifikiri uamuzi juu ya dogma utamaliza
mabishano, lakini haikuwa hivyo, kwa sababu Wagiriki wengi, ingawa hawakukubaliana na Arios,
hawakuridhika na msamiati uliotumika kuelezea uhusiano wa Baba na Mwana.

Mtaguso I wa Konstantinopoli (381)

Mtaguso I wa Konstantinopoli ndio wa pili kati ya mitaguso ya kiekumene yaliyofanyika wakati wa
mababu wa Kanisa. Uliitishwa na kaisari Theodosius I ukafanyika Konstantinopoli mwaka 381.
Maaskofu 150 waliohudhuria walilaani aina mbalimbali za uzushi, hasa ule wa Masedoni wa
Konstantinopoli aliyekanusha umungu wa Roho Mtakatifu, wakathibitisha maamuzi ya mtaguso mkuu
wa kwanza (Mtaguso I wa Nisea), uliofanyika mwaka 325.
Hivyo walikiri kwamba Roho Mtakatifu pia, kama vile Yesu Mwana wa Mungu, anachanga dhati ileile
ya Baba.
Pamoja na hayo, walikamilisha kanuni ya imani ya Nisea ambayo kwa sababu hiyo inaitwa sasa
kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli na ambayo inatumika sana hata leo katika madhehebu
mbalimbali ya Ukristo, hasa katika liturujia.

Mtaguso wa Efeso (431)

Mtaguso wa Efeso unahesabiwa na Wakristo walio wengi kama mtaguso mkuu wa tatu. Ulifanyika
Efeso katika mkoa wa Asia Ndogo, kwa amri ya kaisari Theodosi II; Papa Selestini I (422-432)
alimteua Sirili wa Aleksandria kuuendesha; washiriki walikuwa zaidi ya 150 na kujadili vikali hasa
uzushi wa Nestori wa Konstantinopoli.
Patriarki huyo alikuwa anasisitiza ubinadamu wa Yesu Kristo kuliko umungu wake, akisema Bikira
Maria alimzaa mtu Yesu, si Mungu, wala si Neno wa Mungu aliyehifadhiwa ndani ya nafsi ya Kristo
kama hekaluni. Kwa hiyo Kristo alikuwa Theophoros, yaani "mbeba Mungu", na Maria Christotokos,
"Mama wa Kristo" si Theotokos, "Mama wa Mungu".
Mtaguso huo ulilaani haraka mafundisho hayo ukikiri kwamba nafsi ya Yesu Kristo ni moja tu, ile ya
milele ya Mwana wa Mungu, na kwamba nafsi hiyo ilitwaa ubinadamu kamili wenye mwili na roho.
Hivyo Maria ni Theotokos kwa kuwa alimzaa Mungu kama binadamu.
Wajumbe wa Papa walipofika walithibitisha uamuzi huo, lakini maaskofu kutoka Antiokia
hawakuridhika, na uzushi huo uliendelea Mesopotamia na kuenea hata Asia mashariki.
Mtaguso ulitangaza kuwa Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli ni kamili ukakataza
isibadilishwe kwa namna yoyote. Pia ulilaani Upelaji, uzushi kutoka Ulaya magharibi kuhusu uwezo wa
binadamu kutenda mema bila kusaidiwa na neema ya Mungu.

Mtaguso wa Kalsedonia (451)

Mtaguso wa Kalsedonia (leo katika nchi ya Uturuki) unahesabiwa na Wakristo wengi kuwa wa nne
kati ya mitaguso ya kiekumeni iliyofanyika katika historia ya Kanisa.
Mtaguso huo uliitishwa na kaisari Marcianus wa Dola la Roma Mashariki pamoja na mke wake
Pulkeria wa Bizanti miaka 20 baada ya Mtaguso wa Efeso.
Hao waliona haja ya kudumisha umoja wa Wakristo, uliokuwa msingi wa uimara wa dola hilo, hasa
wakati huo ambapo makabila yasiyo na ustaarabu kutoka Asia yalikuwa yanajaribu kuteka Ulaya.
Umoja huo uliingia hatari ya kuvunjika kutokana na uamuzi wa mtaguso mkuu wa Efeso kuhusu
imani sahihi juu ya Yesu Kristo kutoeleweka kwa namna moja.
Hasa baadhi ya walioshinda mtaguso huo walionekana kusisitiza mno umungu wake hata kutia
shaka kama wanaamini sawasawa ubinadamu wake.
Vikao vilianza tarehe 8 Oktoba 451 vikiwa na washiriki zaidi ya 350: mara nyingi inatajwa idadi ya
600 hivi. Hatimaye mafundisho ya Eutike na Dioskoro wa Aleksandria yalilaaniwa.
Ufanisi wa mtaguso ulichangiwa na msimamo wa kaisari Valentiniano III wa Dola la Roma
Magharibi, binamu wa Pulkeria. Kaisari huyo alimuunga mkono Papa Leo I (440-461) aliyekuwa
ametoa msimamo wake na wa Kanisa la Roma tangu mwaka 449 katika Tomus ad Flavianum, yaani
Waraka kwa Flaviano, Patriarki wa Konstantinopoli aliyeuawa na wafuasi wa Eutike.
Page 2 of 21


3
Ingawa msimamo huo wa kati ulikubaliwa na wengi, wengine waliuona ni kinyume cha uamuzi wa
Efeso, hivyo walishikilia sana mtazamo hao hata walipodhulumiwa na serikali. Ndiyo asili ya farakano la
Misri, Syria, Armenia n.k. linalodumu hata leo.
Mtaguso huo ulitunga pia kanuni mbalimbali, kama vile kwa kumpatia Patriarki wa Konstantinopoli
nafasi ya pili kati ya maaskofu wote.

Mtaguso II wa Konstantinopoli (553)

Mtaguso II wa Konstantinopoli uliitishwa na kaisari Justiniani I mwaka 553 kwa lengo la
kupatanisha tena na Kanisa Katoliki Wakristo wote wa Misri, Syria n.k. waliojitenga miaka 100 iliyopita
kufuatana na Mtaguso wa Kalsedonia.
Kwa ajili hiyo kaisari huyo alifanya yalaaniwe maandishi ya Wanestori watatu (Teodoro wa
Mopsuestia, Teodoreto wa Kiro na Iba wa Edesa) yaliyochukiwa sana na Wamisri.
Pia mtaguso mkuu huo ulilaani baadhi ya mafundisho wa Origene.
Walihudhuria maaskofu 168; kati yao 11 walitokea magharibi. Kumbe Papa Vigili (537-555) na
maaskofu wengine 12 wa magharibi walikataa kuhudhuria ingawa walikuwepo Konstantinopoli, ila
mwaka uliofuata alikubali maamuzi ya mtaguso.
Hatimaye Papa Gregori I (590-604) aliutambua kama mtaguso mkuu kwa sababu haukuharibu kitu.
Hivyo Wakristo wengi wanauhesabu kuwa wa tano kati ya mitaguso ya kiekumeni, ingawa lengo
halikufikiwa, kwa kuwa Wamisri waliendelea kukataa Mtaguso wa Kalsedonia.

Mtaguso III wa Konstantinopoli (680-681)

Mtaguso III wa Konstantinopoli unahesabiwa na Wakristo wengi kuwa wa sita kati ya Mitaguso ya
kiekumeni.
Kaisari Konstantino IV wa Konstantinopoli ndiye aliyeuitisha na kuuendesha kuanzia tarehe 7
Novemba 680 hadi tarehe 16 Septemba 681.
Suala kuu lililosumbua Wakristo wa karne VII lilimhusu Yesu Kristo upande wa utashi. Ulikuwa
unaenea mtazamo wa kwamba hakuwa na utashi wa kibinadamu, bali ule wa Kimungu tu.
Lakini wamonaki Sofronio wa Yerusalemu na Maksimo Muungamadini walipinga vikali jaribio hilo la
kuleta upatanisho wa Waorthodoksi wa Mashariki (Wamisri n.k.) kwa kumpunguza Yesu katika
ubinadamu wake kamili uliosisitizwa na Mtaguso wa Kalsedonia (451).
Vilevile Papa Martin I (649-655), katika mtaguso uliofanyika Laterani, alilaani mtazamo huo,
kinyume cha Kaisari na Patriarki wa Konstantinopoli.
Konstantino IV alikubaliana na Papa Agatoni (678-681), na hivyo Mtaguso III wa Konstantinopoli
ulilaani rasmi mtazamo wa kwamba Yesu hakuwa na utashi wa kibinadamu.

Mtaguso II wa Nisea (787)

Mtaguso II wa Nisea uliitishwa na malkia Irene wa Bizanti mwaka 787 ili kujadili matumizi ya
sanamu katika Ukristo, kutokana na ombi la Papa Adrian I (772-795).
Wakristo wengi wanauhesabu kuwa wa saba kati ya Mitaguso ya kiekumeni. Ni wa mwisho
kufanyika wakati wa mababu wa Kanisa.
Mtaguso mkuu huo ulihitajika ili kumaliza mabishano makali kuhusu sanamu za Kikristo
yaliyochukua zaidi ya miaka 100 hasa katika Dola la Roma Mashariki yakimalizika mwaka 843 tu.
Chanzo ni uamuzi wa kaisari Leo III wa Konstantinopoli (717-741) wa kuteketeza sanamu zote ili
kujilinganisha na Waislamu waliotishia utawala wake.
Patriarki wa Konstantinopoli alilazimika kujiuzulu, lakini uamuzi wa kaisari ulizidi kupingwa hasa na
wamonaki na mwanateolojia Yohane wa Damasko. Mapapa wa Roma pia walipinga uamuzi huo.
Sera ya dola ilibadilika aliposhika uongozi Irene kwa niaba ya mtoto wake mdogo Konstantino VI.
Mtaguso ulianza Konstantinopoli mwaka 786, lakini ulipoingiliwa na jeshi waliowaunga mkono
maaskofu wengi waliopinga sanamu, Irene aliuhamishia Nisea ambapo vilifanyika vikao 7 kuanzia
tarehe 28 Septemba 787. Cha mwisho kilifanyika katika ikulu tarehe 23 Oktoba 787.
Pamoja na maaskofu 300 hivi wa dola hilo, walihudhuria wamonaki wengi. Papa alituma mabalozi
wake wawili na barua moja.
Mtaguso ulitofautisha heshima inayokubalika kwa sanamu na ibada isiyovumilika. Hoja kuu ni
kwamba sanamu si kitu, ila inamwakilisha yule aliyechorwa ndani yake. Kimsingi sanamu zinakubalika
kutokana na umwilisho wa Mwana wa Mungu uliomfanya atwae sura na kuonekana.
Mtaguso ulichukua pia maamuzi mbalimbali ili kurekebisha Kanisa.

Mtaguso IV wa Konstantinopoli (869-870)

Mtaguso IV wa Konstantinopoli ni jina linalotumiwa na Wakristo kwa namna tofauti, kadiri
wanavyokubali au kukataa uhalali na uekumeni wa mitaguso fulanifulani.
Kanisa Katoliki linahesabu kuwa Mtaguso Mkuu IV wa Konstantinopoli ule uliofanyika tangu tarehe 5
Oktoba 869 hadi 28 Februari 870.
Uliitishwa na Kaisari Basili I wa Konstantinopoli na Papa Adrian II (867-872), kwa sababu mwisho
wa ikonoklastia katika sinodi ya mwaka 843 ulikuwa umeacha athari kubwa katika Kanisa la Mashariki.
Page 3 of 21


4
Patriarki Metodi wa Konstantinopoli (843-847) alijitahidi kutuliza pande zote, lakini hakufaulu.
Alipofariki, malkia Teodora, akitawala kwa niaba ya mtoto Mikaeli III, alilazimisha nafasi yake
ishikwe na Ignas I, mmonaki mwenye msimamo mkali, ambaye hatimaye aliondoshwa.
Badala yake alichaguliwa mlei msomi Fosyo ambaye kwa siku chache alipewa daraja na kutawazwa,
lakini kufikia Februari 859 lililotea farakano kati ya waliomkubali yeye na waliomkubali Ignas I.
Ndipo Fosyo alipojitahidi kuungwa mkono na Papa Nikolaus I (858-867), ambaye kwanza alimkubali
pamoja na pendekezo la Kaisari Mikaeli III la kuitisha mtaguso uliofanyika Konstantinopoli kati ya Aprili
na Agosti 861 wakihudhuria maaskofu zaidi ya 300.
Papa hakupendezwa na maamuzi ya mtaguso huo, akashindana na Kaisari kimaandishi kwa sababu
za kiutamaduni na za kisiasa pia.
Hapo Fosyo alipata nguvu dhidi ya Papa akaitisha mtaguso uliovunja umoja kati ya Makanisa ya
Mashariki na yale ya Magharibi mwaka 867, akithubutu kwa mara ya kwanza kumhukumu Papa kama
mzushi na kutaka kumuondoa madarakani.
Kumbe Kaisari mpya alimrudisha Ignas I kuwa Patriarki na pamoja naye akamuomba Papa atume
mabalozi kwa mtaguso mwingine wa kufanyika Konstantinopoli.
Mtaguso ulipoanza tarehe 5 Oktoba 869 walikuwepo tu maaskofu wakuu 5 na maaskofu wengine 7,
lakini walikuwepo mabalozi wa Mapatriarki wa Antiokia na Yerusalemu (wale wa Aleksandria walifika
baadaye).
Waliokuwa upande wa Fosyo walikubaliwa kuhudhuria kuanzia tarehe 7 Oktoba wakamtetea sana
dhidi ya msimamo wa Papa, lakini wakashindwa na kutengwa (29 Oktoba).
Baada ya miezi mitatu mtaguso uliendelea tarehe 12 Februari 870, wakiwepo maaskofu 67
walioongezeka tena hadi kufikia 103 siku ya mwisho (28 Februari), lilipotolewa tamko la imani pamoja
na kanuni 26 kuhusu teolojia na sheria, bila kutoa mafundisho mapya. Pamoja na idadi yenyewe
kutokuwa kubwa sana, ni muhimu kwamba walikuwepo maaskofu wakuu 37 kati ya 40.
Kwa kuwa mtaguso huu haukukubaliwa sana huko Konstantinopoli (hasa baada ya Fosyo kurudia
Upatriarki mwaka 877), na pande mbili zilishindwa zaidi na zaidi kuelewana, uliitishwa mtaguso
mwingine, ambapo wafuasi wa Fosyo walikuwa ndio wengi.
Baadhi ya Waorthodoksi wanahesabu mtaguso huo mpya (879-880), uliofuta maamuzi dhidi ya
Fosyo, kuwa wa kiekumeni na kuukataa ule wa miaka 10 ya nyuma. Lakini wengine hawakubali kuwa
wa kiekumeni kwa sababu haukutoa mafundisho ya imani.
Ingawa wajumbe wa Papa Yohane VIII (872-882) walikubali kwanza maamuzi wa mtaguso huo ili
kudumisha amani, na labda hata yeye mwenyewe, waandamizi wake waliukataa, na Fosyo mwenyewe
aliondoshwa tena mwaka 886.

Mtaguso I wa Laterano (1123)

Mtaguso I wa Laterano unahesabiwa na Kanisa Katoliki mtaguso mkuu wa tisa katika historia yake,
wa kwanza kufanyika Magharibi. Ulianza tarehe 18 Machi ukamalizika tarehe 11 Aprili 1123.
Mahali pake ni kwenye Kanisa Kuu la Roma (Italia) katika mtaa wa Laterano, alipokuwa anaishi
askofu wake. Hukohuko baadaye ilifanyika mitaguso mingine minne ya Karne za Kati, halafu umuhimu
wake ukapungua Papa alipohamia Vatikano.
Mtaguso uliitishwa na Papa Kalisti II (1119-1124) mnamo Desemba 1122, mara baada ya Mapatano
ya Worms, ya kwanza kufanyika kati ya Papa na Dola Takatifu la Kirumi, iliyofurahisha sana
wanakanisa, hata mwaka huo ulitajwa kuwa mwanzo wa kipindi kipya.
Mapatano hayo yalikomesha desturi ya walei kuteua viongozi wa Kanisa na wa utawa,
yakitenganisha shughuli za kiserikali na zile za kidini, na kukubali kwamba mamlaka ya kiroho
inatokana na daraja takatifu.
Ili kuthibitisha mapatano hayo, Papa alialika Roma maaskofu wote wa Magharibi. Waliohudhuria
kweli walikuwa zaidi ya 900 kati ya maaskofu zaidi ya 300 na maabati 600 hivi). Papa mwenyewe
aliendesha vikao.
Hakuna hati za mtaguso, ila matunda yake. Tunachojua ni kwamba Mapatano hayo yalisomwa
yakapitishwa rasmi, pamoja na kanuni 22 au 25, ambazo nyingi zilikuwa zimeshapitishwa zamani.

Mtaguso II wa Laterano (1139)

Mtaguso II wa Laterano, uliofanyika kuanzia tarehe 4 hadi 11 Aprili 1139 chini ya Papa Inosenti II
(1130-1143), unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa mtaguso mkuu wa kumi. Ni wa pili kufanyika
Magharibi, kwenye Kanisa kuu la Roma (Italia).
Mtaguso ulihitajika kutokana na farakano lililotokea mwaka 1130 alipofariki Papa Honori II (1124-
1130): hapo makardinali waligawanyika kuhusu Mapatano ya Worms, ambayo mwaka 1122 yalikuwa
yamekomesha mashindano kuhusu uteuzi wa maaskofu.
Isitoshe, kulikuwa na ushindani kati ya koo mbili za Roma, yaani Frangipane na Pierleoni.
Tarehe 14 Februari 1130, makardinali 16 waliosimama upande wa familia ya Frangipane
walimchagua Gregorio Papareschi, aliyejiita Papa Inosenti II. Saa chache baadaye, Pietro Pierleoni
alichaguliwa na makardinali wengine na kujiita Anakleti II.
Hatimaye, kwa msaada wa Bernardo wa Clairvaux, Inosenti II alishinda na kukubaliwa na wengi,
ingawa hakuweza kuhamia Roma mpaka baada ya mpinzani wake kufa (1138).
Page 4 of 21


5
Mtaguso ulipaswa kurekebisha matokeo ya farakano hilo. Basi, Inosenti II alifungua kikao na
kuondoa madarakani maaskofu waliomfuata mpinzani wake.
Halafu papa alikusudia kuendeleza juhudi za urekebisho za Mtaguso I wa Laterano. Hivyo
zikapitishwa kanuni 30, ambazo nyingi kati yake zilikuwa za kurudia zile za zamani kuhusu usimoni,
mapadri wenye wake n.k.

Mtaguso III wa Laterano (1179)

Mtaguso III wa Laterano uliitishwa na Papa Aleksanda III (1159-1181) ufanyike huko Roma mwaka
1179, kutokana na Amani ya Venezia kati ya Kaisari Federiko I wa Ujerumani na Lega Lombarda ya
Italia kaskazini.
Unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na moja. Ulijadili masuala
mbalimbali na kuyatungia kanuni. Kati ya maamuzi muhimu zaidi, mmojawapo ulihusu uchaguzi wa
Papa, ukidai thuluthi mbili za kura za makardinali wote, bila kutofautisha haki za makundi yao matatu.

Mtaguso IV wa Laterano (1215)

Mtaguso IV wa Laterano unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na mbili.
Uliitishwa na Papa Inosenti III (1198-1216) kama kilele cha kazi yake.
Ulihudhuriwa na maaskofu zaidi ya 400 (wakiwemo mapatriarki wa Kilatini wa Konstantinopoli na
Yerusalemu na wawakilishi wa wale wa Antiokia na Aleksandria), na wakuu wa watawa zaidi ya 800,
mbali na mabalozi wa watawala wa nchi mbalimbali.
Mada kuu zilikuwa Vita vya msalaba, Mashindano kuhusu uteuzi wa viongozi wa Kanisa, mamlaka
ya Papa, mwenendo wa makleri, mashirika ya kitawa, imani (kuhusu ekaristi n.k.) na wajibu wa
Wakristo wote kupokea sakramenti ya kitubio walau mara moja kwa mwaka.
Kutokana na wingi na umuhimu wa mafundisho na maamuzi yaliyotolewa, mtaguso huo
unahesabiwa kuwa kati ya ile iliyoathiri zaidi Kanisa hadi leo.

Mtaguso I wa Lyon (1245)

Mtaguso I wa Lyon uliitishwa na Papa Inosenti IV (1243-1254) tarehe 24 Juni 1245 akiwa huko
Lyon (Ufaransa), alipokimbilia usalama. Waliushiriki karibu viongozi 150 wa Kanisa Katoliki, ambalo
linauhesabu kuwa mtaguso mkuu wa kumi na tatu.
Baada ya mashindano makali kati ya mamlaka ya kiroho ya Papa na ile ya kisiasa ya kaisari huko
Ulaya, mtaguso huo uliitishwa ili kumhukumu moja kwa moja kaisari Federiko II kuwa Mpinga Kristo.
Mtaguso ulianza tarehe 28 Juni 1245 wakiwepo maaskofu 144, halafu ukawa na vikao viwili vingine
tena tarehe 5 Julai na 17 Julai. Hatimaye maaskofu walikuwa 225.
Mwanzoni papa alitangaza matatizo 5 yanayotesa Kanisa:
 •  kuharibika kwa imani na maadili;
 •  kushindwa kuikomboa Nchi takatifu (Yerusalemu ulitekwa tena na Waturuki mwaka 1244);
 •  kudumu kwa farakano la Waorthodoksi;
 •  kujitokeza hatari ya kuvamiwa na Watartari;
 •  kupambana na Federiko II.
Maamuzi yalitangazwa tarehe 25 Agosti tu, baada ya papa na wasaidizi wake kurekebisha miswada,
yakapokewa na kufafanuliwa na vyuo vikuu. Lakini uamuzi wa kumuondoa madarakani kaisari
haukuweza kutekelezwa hata kwa vita.

Mtaguso II wa Lyon (1274)

Mtaguso II wa Lyon unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na nne.
Ulikusudiwa hasa kurudisha umoja kamili kati ya Wakatoliki na Waorthodoksi, uliotafutwa katika karne
XIII yote.
Mnamo Februari 1274, katika ikulu ya Konstantinopoli, kaisari Mikaeli VIII ilifaulu kufanya maaskofu
wengi wakiri ungamo la imani lililodaiwa na Papa Klementi IV (1265-1268).
Ndipo Papa Gregori X (1271-1276) alipoitisha mtaguso huko Lyon, ambao uhudhuriwe na
wawakilishi wa Waorthodoksi ili kukamilisha umoja.
Papa Gregori X alifungua mtaguso tarehe 7 Mei 1274 akitangaza tena malengo yake matatu:
 •  kusaidia Wakristo wa Nchi takatifu,
 •  kuungana tena na Waorthodoksi,
 •  kurekebisha maadili ndani ya Kanisa.
Vilifuata vikao viwili tarehe 18 Mei na 4 Juni. Halafu tarehe 24 Juni ulifika na kupokewa kwa
shangwe ujumbe kutoka Ugiriki, ukiundwa na maaskofu 2 na katibu wa kaisari.
Tarehe 6 Julai kilifanyika kikao cha nne kwa ajili ya muungano na hatimaye tarehe 16 Julai kile cha
mwisho kilichopitisha hati mbalimbali za urekebisho. Kesho yake mtaguso ulifungwa.
Muungano haukuweza kudumu, kwa sababu, alivyoandika Papa Paulo VI (1963-1978) tarehe 19
Oktoba 1974, ulifanyika «bila kulipatia Kanisa la Kigiriki nafasi ya kutokeza kwa hiari mtazamo wake
kuhusu jambo hilo. Wakristo wa Kilatini ndio waliotunga hati na matamko kufuatana na mafundisho
juu ya Kanisa yaliyofafanuliwa na kupangwa magharibi».
Page 5 of 21


6
Mikaeli VIII alijaribu kulazimisha raia zake wapokee mambo wasiyoyakubali kwa moyo, hata
akatumia nguvu kuwadhulumu waliokataa; akilaumiwa na watu wa Roma kwa kushindwa kufanikisha
muungano, akaja kutengwa na Kanisa. Alipokufa (1282), mwanae Androniko II aliyemrithi, alifuta
maamuzi ya baba yake kwa ajili ya muungano.
Vilevile mipango kwa ajili ya vita vya msalaba haikutekelezwa, na hatimaye (1291) Waturuki
waliteka Akri, mji wa mwisho kubaki mikononi mwa Wakristo huko Mashariki ya Kati.
Maamuzi mengine yalihusu utaratibu mpya wa kumchagua Papa kwa lengo la kuzuia uchelewaji
uliojitokeza hapo nyuma, na katazo la mashirika mapya ya kitawa.

Mtaguso wa Vienne (1311-1312)

Mtaguso wa Vienne unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi na tano.
Mtaguso huu ulifanyika Vienne (Ufaransa) baada ya mashindano kati ya Papa Bonifas VIII (1294-
1303) na mfalme wa Ufaransa Filipo IV.
Hatimaye mwaka 1309 mwandamizi wake, Papa Klementi V (1305-1314) alikubali kubaki Avignon
(leo nchini Ufaransa), karibu na himaya ya mfalme huyo.
Mapapa walibaki huko hadi mwaka 1377, waliporudi Roma.
Kwa shinikizo la mfalme, Papa alitoa hati Regnans in excelsis (12 Agosti 1308) ili kuitisha mtaguso
mkuu huko Vienne tarehe 1 Novemba 1310, kwa lengo la kujadili mada 4:
 •  suala la Wahekalu;
 •  vita vya msalaba;
 •  hali ya imani na Kanisa kwa jumla;
 •  urekebisho wa Kanisa.
Mtaguso ulichelewa kuanza hadi tarehe 16 Oktoba 1311, walipokuwepo washiriki 170 hivi, ambao
kati yao Wafaransa walikuwa zaidi ya thuluthi moja. Wengine walizuiwa na mfalme wa Ufaransa.
Vikao rasmi vikawa vitatu hadi Machi 1312.
Kuhusu Wahekalu, mtaguso uliamua kufuta shirika lao kama alivyopenda mfalme, bila kulifanyia
utafiti wala kulitolea hukumu.
Kuhusu Vita vya Msalaba, uliamua kuvianza upya na kwa ajili hiyo kutoza zaka kwa miaka sita,
lakini mfalme alijitwalia hizo pesa bila kutekeleza ahadi yake ya kuongoza vita hivyo.
Kuhusu imani, ulijadili baadhi ya mafundisho hasa ya makundi kadhaa ya watawa, lakini uamuzi
ulichukuliwa baadaye tu.
Kuhusu urekebisho, ulidai haki za Kanisa ziheshimiwe na serikali za nchi. Pia ulijadili kirefu
mahusiano ya ndani, hasa kati ya maaskofu, maparoko na watawa.

Mtaguso wa Konstanz (1414-1418)

Mtaguso wa Konstanz (Ujerumani) unahesabiwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa kumi
na sita. Uliitishwa na antipapa Yohane XXIII kwa ombi la kaisari Sigismund wa Ujerumani
ukathibitishwa na Papa Gregori XII (1406-1415).
Lengo kuu lilikuwa kumaliza Farakano la Magharibi lililofikia hatua ya kuona maaskofu watatu
kujidai Papa kwa wakati mmoja. Malengo mengine yalikuwa kung’oa uzushi na kurekebisha Kanisa
“katika kichwa na viungo vyake”.
Hatimaye Papa Gregori XII alikubali kujiuzulu, wapinzani wake wawili waliondolewa, na Papa Martin
V akachaguliwa.
Ulikuwa mtaguso muhimu kwa wingi wa waliohudhuria (makardinali 29, maaskofu 186, maabati
zaidi ya 100 na wataalamu 300 hivi), muda (vikao 55) na mafanikio, ingawa majaribio yake ya
mapinduzi yalishindikana, hasa ulipodai kuwa na mamlaka ya juu kuliko Papa.
Kati ya maamuzi mengine kuna hukumu dhidi ya John Wyclif na Jan Hus kama wazushi.

Mtaguso wa Firenze (1431-1445)

Mtaguso wa Firenze uliitishwa na Papa Martin V (1417-1431) mwaka wa mwisho wa uongozi wake
ili kutekeleza shingo upande agizo la Mtaguso wa Konstanz la kwamba mtaguso ufanyike mara kwa
mara.
Mtaguso ulianza Basel (Uswisi) chini ya Papa Eugenio IV (1431-1447), ukiwa na maaskofu
wachache kulingana na mapadri na walei wenye haki ya kupiga kura.
Ingawa mtaguso ulifaulu kupatanisha wafuasi wa Hus na Kanisa, na kutoa sheria kadhaa za
urekebisho kwa kibali cha Papa, baadaye ulianza kumshambulia yeye pamoja na makardinali,
ukionyesha wazi wengi waliuona una mamlaka ya juu kuliko Papa, kinyume cha mapokeo.
Hapo Eugenio IV aliuvunja halafu akauhamishia Ferrara (Italia), ulipokutanika tarehe 8-1-1438, bila
kujali upinzani wa wale ambao walibaki Basel na kumchagua antipapa wa mwisho, Felix V.
Huko Italia ulifika ujumbe mkubwa kutoka Konstantinopoli kwa ajili ya kurudisha umoja kati ya
Kanisa Katoliki na Waorthodoksi. Kati ya wajumbe 700 kulikuwa na kaisari na patriarki wa
Konstantinopoli, walioogopa Waturuki watateka mji wao (kama ilivyotokea kweli tarehe 29 Mei 1453);
hivyo walihitaji msaada wa Wakristo wenzao wa magharibi.
Ferrara iliachwa kutokana na uhaba wa majengo na hofu ya tauni.
Page 6 of 21


7
Mwaka 1439 mtaguso ulihamia Firenze ukafikia makubaliano ya kurudisha umoja (6-7-1439),
ingawa uamuzi ukashindwa kutekelezwa kwa kiasi kikubwa kutokana na upinzani wa waumini wa
Konstantinopoli.
Vilevile tarehe 22-11-1439 yalifikiwa makubaliano na Waarmenia na tarehe 4-2-1440 yale na
Wamisri.
Hatimaye tarehe 24-9-1443 mtaguso ulihamia Roma kwenye Laterano. Huko yalifikiwa makubaliano
ya kurudisha umoja na Wasiria kadhaa (30-4-1444) na Wakaldayo na Wamaroni wa Kupro (7-8-1445).
Hakuna hati kuhusu mwisho wa mtaguso. Lakini waliobaki Basel na kujitenga na Papa, kufikia
tarehe 19-4-1449 walimkubali Nikolaus V na siku sita baadaye walifunga mkutano wao.
Mtaguso huo ulichochea Wakristo wa magharibi kutamani mawasiliano na wenzao wa Ethiopia na
India, jambo lililowafanya waanze zile safari za mbali kupitia baharini zilizowafikisha Afrika Kusini na
Mashariki, China na Amerika.

Mtaguso V wa Laterano (1512-1517)

Mtaguso V wa Laterano ulifanyika kuanzia mwaka 1512 hadi 1517 huko Roma. Kanisa Katoliki
linauhesabu kama mtaguso mkuu wa kumi na nane.
Uliitishwa na Papa Julius II (1503-1513) ambaye alianza kuusimamia tarehe 3 Mei 1512. Baada ya
kifo chake, uliendelezwa na Papa Leo X (1513-1521) hadi kikao cha 12 na cha mwisho kilichofanyika
tarehe 16 Machi 1517.
Ulihudhuriwa na maaskofu 100 hivi, wengi wao wakitokea Italia. Kutofika kwa wajumbe kutoka nchi
nyingine, pamoja na wengi kukosa nia ya kujirekebisha, kulichangia kufanya utekelezaji wa maamuzi
ya mtaguso ushindikane.
Maamuzi hayo yalitolewa kwa hati za Papa. Mengine yanahusu mafundisho ya imani, mengine
maagizo ya urekebisho wa Kanisa.
Kabla yake kilifanyika "Kitaguso" cha Pisa: kwa kuwa Papa Julius II alikuwa hatekelezi kiapo chake
cha kuitisha mtaguso kwa ajili ya urekebisho, baadhi ya makardinali, wakihimizwa na watawala wa
Ujerumani na Ufaransa, waliuitisha huko Pisa (Italia) kuanzia tarehe 1 Septemba 1511. Walikusanyika
wachache tarehe 1 Oktoba, halafu katika kikao cha nane walimsimamisha Papa wakahamia Lyon
(Ufaransa).
Papa aliitikia “kitaguso” hicho kwa hati ya tarehe 18 Julai 1511, ambayo pamoja na kukipinga na
kujitetea aliitisha mtaguso mkuu ukusanyike tarehe 19 Aprili 1512 huko Laterano.
Vita vilichelewesha mwanzo wa mtaguso wenyewe hadi tarehe 3 Mei 1512, walipokusanyika katika
basilika la Laterano makardinali 15, mapatriarki 2, maaskofu wakuu 10, maaskofu 56, maabati na
wakuu wa mashirika ya kitawa wachache pamoja na mabalozi wa nchi 3. Mwisho walikuwepo
makardinali 23 na maaskofu 122.
Upande wa matokeo, utekelezaji wa maagizo ya mtaguso ulikuwa mdogo sana, la sivyo pengine
Matengenezo ya Kiprotestanti yasingetokea. Ukweli ni kwamba Martin Luther aliyaanzisha miezi sita tu
baada ya mtaguso kwisha.

Mtaguso wa Trento (1545-1563)

Mtaguso wa Trento (uliofanyika kwa kwikwi kuanzia mwaka 1545 hadi 1563), unahesabiwa na
Kanisa Katoliki kuwa mtaguso mkuu wa kumi na tisa.
Mtaguso huo, uliochukua muda mrefu kuliko yote ya historia, ulieneza urekebisho wa Kanisa na
kuchukua msimamo kuhusu mafundisho ya Waprotestanti waliojitokeza katika hiyo karne XVI.
Mtu wa kwanza kulilia mtaguso ambao uamue kati yake na papa alikuwa Martin Luther (1517):
huko Ujerumani ombi lake liliungwa mkono na wengi, pamoja na kaisari Karolo V aliyeuona kuwa njia
ya kurekebisha Kanisa lakini pia ya kujiimarisha kimamlaka. Ndiyo sababu kuu iliyomfanya Papa
Klementi VII (1523-1534), aliyesimama upande wa Ufaransa, kukataa kabisa kuuitisha.
Wazo hilo lilipata nguvu tena chini ya mwandamizi wake, Papa Paulo III (1534-1549), ambaye
mwaka 1536 aliitia kwanza Mantova halafu Vicenza maaskofu na maabati wote, pamoja na wafalme
wadogo wengi wa Dola takatifu la Kijerumani.
Baada ya juhudi mbalimbali kushindikana, mwaka 1542 uamuzi ulifikiwa wa kuitisha mtaguso huko
Trento kwa sababu ni mji wa Italia lakini ulikuwa ndani ya mipaka ya dola hilo. Hatimaye (Novemba
1544) papa aliweza kutoa hati ya kuitisha mtaguso inayoitwa Laetare Jerusalem.
Mtaguso ulifunguliwa rasmi tarehe 13 Desemba 1545 katika kanisa kuu la Mt. Vigilio.
Mwanzoni mtaguso ulikuwa na maaskofu wachache, karibu wote kutoka Italia, ukatawaliwa na
wajumbe wa papa. Kati ya makardinali wapya (Contarini, Sadoleto, Carafa, Fisher na huyo Pole) wengi
walipenda urekebisho.
Zilijadiliwa na kupitishwa hasa dogma dhidi ya mafundisho ya Waprotestanti, kama vile kuhusu
utakaso na wokovu. Pamoja na kupitisha tafsiri rasmi ya Biblia katika Kilatini iliyo maarufu kwa jina la
Vulgata, kati ya maamuzi muhimu zaidi upo ule wa kudai maaskofu waishi katika majimbo yao ili
kufanya uchungaji uliowapasa.
Baada ya mtaguso kuhamishiwa Bologna, Papa Paulo III aliusimamisha mnamo Septemba 1549.
Papa Julius III (1550-1555) aliuitisha tena kuanzia tarehe 1 Mei 1551 na zikatolewa hati juu ya
sakramenti za Ekaristi, Kitubio na Mpako wa wagonjwa. Polepole waliohudhuria waliongozeka,
Page 7 of 21


8
wakiwemo Waprotestanti wengi pia, wakidai wanateolojia wao wawe na haki ya kupiga kura na hati
zilizokwishatolewa zifutwe. Ndipo ilipoonekana wazi kwamba tofauti katika imani ni kubwa mno.
Majeshi ya Kiprotestanti yalipokaribia Trento, Papa alikubali kusimamisha tena mtaguso tarehe 28
Aprili 1552.
Sehemu ya mwisho ya mtaguso baada ya kuitishwa ilichelewa kuanza hadi tarehe 18 Januari 1562,
tena ilikabili matatizo mengi, lakini iliokolewa na kutawaliwa na askofu wa Milano Karolo Borromeo,
mpwa wa Papa Pius IV (1559-1565) aliyemalizia haraka mtaguso wakiwemo wajumbe 255.
Katika sehemu hiyo yalitolewa mafundisho rasmi kuhusu Misa, Daraja takatifu na Ndoa, Toharani,
sala kwa watakatifu, heshima kwa masalia na rehema. Pia Kanisa la Roma lilikubaliwa kama mama na
mwalimu wa makanisa yote. Maaskofu wote walitakiwa kuahidia utiifu kwa Papa, ambaye peke yake
ana haki ya kuitisha mtaguso mkuu. Kwa msingi huo, mtaguso ulimuachia Papa kuthibitisha maamuzi
yote, naye alifanya hivyo bila kujali upinzani wa maofisa wake huko Roma.
Isitoshe, mwishoni, maamuzi mbalimbali yaliachwa mikononi mwa Papa na ofisi zake,
yakachukuliwa miaka iliyofuata; kati yake, urekebisho wa Breviari na Misale, kwa kusawazisha liturujia
za majimbo ya magharibi (isipokuwa chache, kama ya Milano na Lyon) kulingana na mapokeo ya
Roma. Halafu ikatolewa Katekisimu ya Trento na Orodha ya vitabu vilivyokatazwa (Index librorum
prohibitorum).

Mtaguso I wa Vatikano (1869-1870)

Mtaguso I wa Vatikano unatazamwa na Kanisa Katoliki kama mtaguso mkuu wa ishirini katika
historia yake.
Uliitishwa rasmi na Papa Pius IX (1846-1878) mnamo 29 Juni 1867 na vikao vyake viliendelea
katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikano mjini Roma kuanzia tarehe 8 Desemba 1869 hadi vilipokatika
mnamo 1870, kutokana na jeshi la Italia kuteka Roma tarehe 20 Septemba.
Walishiriki maaskofu na mapadri 774 (kati ya 1050 wenye haki ya kuhudhuria), ambao kwa mara
ya kwanza walitokea mabara yote. Pia ilikuwa mara ya kwanza ya kutokuwepo wawakilishi wa serikali.
Kumbe wajumbe wa Waorthodoksi na wa Waprotestanti walialikwa pia, lakini hawakufika.
Tarehe 24 Aprili 1870, baada ya majadiliano mengi, ilipitishwa hati Dei Filius juu ya Mungu, ufunuo,
imani, na uhusiano kati ya imani na akili.
Ingawa lengo halikuwa hilo, tokeo kuu la kazi ya mtaguso huo ni tangazo la dogma ya Papa kuwa
na karama ya kutokosea katika mafundisho ya imani na maadili anayoyatoa ili yadumu moja kwa moja
pale anapotimiza masharti fulani (kwa kifupi: akisema "ex cathedra", yaani "kutoka ukulu).
Dogma hiyo iliimarisha mamlaka ya Papa na umoja wa Kanisa dhidi ya maelekeo ya kitaifa ambayo
yalitawala karne zilizotangulia yakisababisha matatizo mengi.

Mtaguso II wa Vatikano (1962-1965)

Malengo ya Mtaguso II wa Vatikano
Muda mfupi baada ya kuchaguliwa Papa, mwenye heri Yohane XXIII alitangaza uamuzi wake wa
kuitisha mtaguso mkuu akiamini kwamba utaweza kuandaa na kusababisha ustawi mpya wa maisha ya
Kanisa. Lengo kuu la mtaguso lilikuwa kuliamsha Kanisa likumbuke wito wake na kwa kujifanya upya
kwa ndani lipate msukumo mpya wa kimisionari ili kuwatangazia watu wote ujumbe wa milele wa
wokovu, amani na umoja.
Tangazo hilo lilitolewa tarehe 25-1-1959. Baada ya maandalizi, Mtaguso II wa Vatikano ulifunguliwa
tarehe 11-10-1962. Vikao vinne vikafanyika mpaka ulipofungwa tarehe 8-12-1965. Kila kikao kilianza
Oktoba na kumalizika Desemba ya miaka hiyo.
Kwa kuwa Yohane XXIII alifariki tarehe 2-6-1963, vikao vitatu vya mwisho viliongozwa na
mwandamizi wake, Paulo VI, na hati zote kumi na sita zikatolewa chini yake pia kwa kupigiwa kura ya
ndiyo karibu kwa kauli moja. Maaskofu na wakuu wa mashirika kadhaa wenye haki ya kupiga kura
walikuwa kama elfu tatu, wakiwakilisha karibu Kanisa lote duniani, isipokuwa nchi zile zenye
kuwadhulumu Wakristo.

Orodha ya hati 16 za mtaguso

HADHI JINA LA KILATINI KIFUPISHO YAHUSUYO TAREHE
KATIBA 1. Sacrosanctum Concilium SC Liturujia takatifu 4-12-1963
2. Lumen Gentium LG Kanisa 21-11-1964
3. Dei Verbum DV Ufunuo wa Kimungu 18-11-1965
4. Gaudium et Spes GS Kanisa katika ulimwengu
wa kisasa
7-12-1965
MAAGIZO 1. Inter Mirifica IM Vyombo vya upashanaji
habari
4-12-1963
2. Orientalium Ecclesiarum OE Makanisa katoliki ya
mashariki
21-11-1964
3. Unitatis Redintegratio UR Ekumeni 21-11-1964
Page 8 of 21


9
4. Christus Dominus CD Huduma ya kichungaji ya
maaskofu
28-10-1965
5. Perfectae Caritatis PC Kurekebisha upya maisha
ya kitawa
28-10-1965
6. Optatam Totius OT Malezi ya kipadri 28-10-1965
7. Apostolicam Actuositatem AA Utume wa walei 18-11-1965
8. Ad Gentes AG Utendaji wa kimisheni wa
Kanisa
7-12-1965
9. Presbyterorum Ordinis PO Huduma na maisha ya
kipadri
7-12-1965
MATAMKO 1. Gravissimum Educationis GE Malezi ya Kikristo 28-10-1965
2. Nostra Aetate NA Uhusiano wa Kanisa na
dini zisizo za Kikristo
28-10-1965
3. Dignitatis Humanae DH Uhuru wa dini 7-12-1965
Hati zote za mtaguso zinapatikana katika tafsiri ya Kiswahili: HATI ZA MTAGUSO MKUU WA
VATIKANO II – tafsiri ya Familia za Maamkio – ed. TEC – Baraza la Maaskofu Tanzania – Ndanda 2001
– ISBN 9976-63-649-0

Mapokezi ya mtaguso

Kwa kuwa Roho Mtakatifu alitaka hivyo, Wakristo walio wengi walipokea kazi ya mtaguso kwa
mikono miwili, na wengi nje ya Kanisa pia waliridhika sana. Kutokana nao yamepatikana matunda
mengi, lakini zimejitokeza hata kasoro na shida kwa sababu mbalimbali, hasa kwa kutoelewa wala
kutotekeleza sawasawa maagizo yake. Kwa vyovyote hatuwezi kusema yote yaliyotokea baada ya
mtaguso yamesababishwa nao, k.mf. maovu yaliyofanywa na baadhi ya mapadri hayamo kabisa.
Pamoja na upinzani wa wazi wa mifumo kadhaa ya kisiasa (ukomunisti na ubepari) na matapo
mengine (Wamasoni n.k.) dhidi ya Kanisa, hali ya jumla ya ulimwengu inazidi kuelekea anasa na
kuabudu utajiri hata kuzima maisha ya Kiroho. Hivyo ni vigumu kufanikisha mtaguso.
Hata ndani ya Kanisa wengi wamesoma hati zake kijuujuu, wakishikilia upande mmoja na kutojali
wa pili. Wengine wamevunjika moyo kuona utekelezaji wa mtaguso unavyokwenda polepole. Wengine
wameshughulikia miundo tu ya Kanisa, bila kujali fumbo la Kimungu lililomo ndani yake. Pengine
umekosekana upambanuzi, k.mf. wengi walipofuata mitazamo ya ulimwengu uliomuasi Mungu badala
ya kujadiliana nao ili kuuokoa.
Matatizo yaliyojitokeza baada ya mtaguso yanaonyesha haja ya kuupokea vizuri zaidi, kwa kupiga
hatua nne zifuatazo:
1. Hati za mtaguso zijulikane na watu wengi zaidi na kwa dhati zaidi.
2. Zipokewe kwa moyo.
3. Zizingatiwe kwa upendo.
4. Zitekelezwe maishani.

Namna ya kuelewa mtaguso

Tukitaka kuelewa vizuri hati za mtaguso, ni lazima tuzizingatie zote 16 zilivyo na
zinavyofungamana. Ni lazima pia tutie maanani hasa katiba zake 4, kwa kuwa ndizo hati kuu
zinazotuwezesha kuelewa maagizo 9 na matamko 3. Tena hatutakiwi kutenganisha mtazamo wa
kichungaji na msingi wa imani wa hati hizo, wala kutenganisha roho ya mtaguso na hati zenyewe.
Mwishowe mtaguso ueleweke katika mapokeo ya Kanisa kwa kuwa katika mitaguso yote Kanisa ni
lilelile. Hivyo tu tutapata mwanga tunaouhitaji kwa wakati huu.
Tahadhari hizo zote zinahitajika kwa sababu katika kutekeleza mtaguso yamejitokeza maelekeo
mawili ambayo yanapingana na kuvuruga hali ya Kanisa. La kwanza linadai mabadiliko yasiyolingana
na mtaguso, ingawa wenyewe wanasema ni maendeleo yanayotakiwa na roho ya mtaguso. Maendeleo
ya namna hiyo hayakubaliki kwa sababu hayajali mapokeo ya mitume yanayodai imani idumu kuwa
ileile. La pili linaambatana na mambo ya zamani, bila kujali ishara za nyakati zetu zinazodai mambo
mapya pia kwa wokovu wa watu wa leo na wa kesho.
Ni wajibu wa maaskofu chini ya Papa kutambua yapi yanajenga na yapi yanazuia ujenzi au pengine
yanabomoa Kanisa. Ndiyo kazi inayofanyika hasa katika sinodi (= pamoja-njia, yaani kusafiri pamoja).
Kati ya sinodi za ngazi mbalimbali kuanzia ile ya jimbo, muhimu zaidi ni zile za kimataifa zinazofanyika
mara kwa mara huko Roma (mtaa wa Vatikano), zikikusanya maaskofu wawakilishi wa nchi zote na
baadhi ya wakuu wa mashirika ya kitawa.
Juhudi za kutekeleza mtaguso
Kama vile mitaguso mikuu iliyotangulia kupanga urekebisho wa hali ya Kanisa, Mtaguso II wa
Vatikano pia ujumbe wake hautaweza kuzaa matunda isipokuwa kwa juhudi za muda mrefu. Miaka
ishirini baada ya mtaguso kumalizika, sinodi maalumu iliyoitishwa ili kutathmini matokeo yake ilisema
wazi kuwa kazi bado sana, kwa namna ya pekee kuhusu kulenga utakatifu kwa waamini wote. Ndiyo
maana ilihamasisha tufanye juu chini ili ujumbe wa mtaguso usikilizwe upya katika kila jimbo. Ni
lazima tushike jembe kwa kazi hiyo bila kuangalia nyuma tukipatwa na matatizo yasiyoepukika.
Page 9 of 21


10

Hati za mtaguso mojamoja

SACROSANCTUM CONCILIUM

Kikao cha pili cha mtaguso kilipitisha hati mbili za kwanza. Ya kwanza kabisa inahusu liturujia
ambayo ni moyo wa Kanisa kwa kuwa ndipo linapoungana na Mungu wake na kuonekana katika sura
yake takatifu. Lengo la hati hii ni kufanya kwanza mapadri, halafu Wakristo wengine pia waelewe na
kutimiza liturujia ili kwa njia yake wamtukuze kweli Mungu na kufaidika Kiroho.
Karne XX iliiandaa kwa kuwa wataalamu walijitahidi kwa muda mrefu kuchambua maana ya liturujia
kwa jumla na ya ibada zake mbalimbali. Mapapa wote walipokea na kuagiza marekebisho kadhaa
yalitopendekezwa na wataalamu hao. Lakini kazi kubwa zaidi ilikuwa bado.
Kikwazo kikuu kilikuwa ni lugha ya Kilatini iliyokwishakufa tangu miaka elfu hivi. Muda huo wote
wasomi tu waliweza kuelewa masomo na mengineyo ya liturujia. Hivyo watu wa kawaida wakawa
watazamaji tu wa matendo ya ibada. Bila kupata mafundisho wala sakramenti ya ekaristi, Wakristo wa
magharibi walijitungia ibada zao badala ya kutegemea liturujia ya Kanisa.
Huko mashariki hali ilikuwa tofauti kabisa: ndiyo sababu hati hii inahusu liturujia ya Roma tu,
isipokuwa misingi ya liturujia yoyote na mengineyo yanayofaa hata mashariki.
Sura ya kwanza inahusu kanuni za jumla kwa urekebisho na ustawishaji wa liturujia. Kwanza
inaeleza undani na umuhimu wake, halafu inasisitiza haja ya malezi ya kiliturujia kuanzia seminari na
nyumba za kitawa ambapo maisha yote yafuate roho ya liturujia na masomo yote yafundishwe kwa
kuonyesha uhusiano wake na liturujia ambayo ihesabiwe kati ya masomo muhimu zaidi na
kufundishwa na wataalamu. Hivyo waamini wote watasaidiwa kuchota roho halisi ya Kikristo katika
chemchemi hiyo ya kwanza na ya lazima; pia wataweza kushiriki ibada kwa jinsi iliyo haki na wajibu
wao.
Baadaye tu yanaagizwa marekebisho ya jumla ya liturujia na vitabu vyake vyote; msingi wake ni
kwamba liturujia, mbali ya mambo yaliyoagizwa na Bwana, ina mengi yaliyopangwa na Kanisa lenyewe
katika historia yake kulingana na mahali na nyakati mbalimbali. Kwa hiyo mara kwa mara linaweza na
kupaswa kuyapanga upya kwa manufaa ya waamini.
Kwa kuwa liturujia ni kazi ya Kanisa lote, inaratibiwa na uongozi wake tu: wengine wasithubutu
kubadilisha lolote wanapofanya ibada zake. Hata uongozi wa Kanisa usirekebishe vitabu harakaharaka
na pasipo lazima, bali uhakikishe kwamba mapya yanalingana na ya zamani.
Kwa namna ya pekee ni lazima neno la Mungu katika liturujia liheshimiwe linavyostahili, tena
lionjwe kama ilivyokuwa mwanzoni mwa Kanisa.
Maagizo mengine yanatokana na hali ya kijumuia ya liturujia, yaani kwamba ibada zake si za
binafsi, bali ni za Kanisa lote, na kila mmoja anahusika namna yake kama mwamini wa kawaida au
kama mwenye daraja au huduma fulani. Hivyo ipendelewe ibada ya pamoja ambapo kila mmoja ashike
nafasi yake na kulingana vizuri na wengine wanaoshika nafasi zao.
Maagizo mengine yanazingatia faida ya waamini upande wa imani ikiwa ni pamoja na kujifunza
undani wa imani yenyewe. Kwa ajili hiyo mtaguso umeamua ibada zieleweke kwa urahisi, mapadri
watoe hotuba na mawaidha mbalimbali wakati wa ibada, pia ziruhusiwe lugha hai za watu ingawa
Kilatini kinabaki lugha rasmi ya madhehebu ya Kanisa la magharibi na waamini wake wote
wanatarajiwa kujua kuitikia na kuimba kwa Kilatini wakati wa Misa.
Mbali ya lugha, mtaguso umekubali yafanyike marekebisho mengine ili kupokea katika liturujia ya
Roma utamaduni wa makabila yoyote mradi usipingane na imani. Utamadunisho huo ufanyike chini ya
Baraza la Maaskofu na kukubaliwa na Roma.
Mwisho wa sura hiyo unasisitiza umuhimu wa watu kushiriki liturujia ya askofu katika Kanisa kuu na
ile ya parokia ili waamini wajisikie kweli Kanisa moja.
Ili kustawisha liturujia mtaguso umeagiza ziwepo kamati maalumu kitaifa na kijimbo.
Ili kutekeleza yaliyosemwa hapo juu, sura ya pili inaagiza namna ya kurekebisha madhehebu ya
Misa, sura ya tatu inafanya vilevile kuhusu sakramenti nyingine na visakramenti, na sura ya nne
kuhusu Sala ya Kanisa. Kwa sasa vitabu hivyo vyote tunavyo tayari vimerekebishwa: katika kuvitumia
ni muhimu kujisomea utangulizi wake.
Sura ya tano inarekebisha mwaka wa Kanisa kusudi mpango wake ueleweke zaidi kwa kutojaa
sikukuu za watakatifu wengi mno: hasa siku ya Bwana na vipindi maalumu vya mwaka vipate nafasi
vinavyostahili.
Sura mbili za mwisho zinahusu muziki na sanaa takatifu ili liturujia ipendeze kwa uzuri wake, iinue
roho kwa Mungu na kuwa kielelezo cha ile ya mbinguni. Hivyo vipawa mbalimbali vya binadamu
vitumike kumtukuza Mungu. Hayo yameelezwa baada ya vitabu kwa sababu hivyo vina neno la Mungu
na maitikio yetu kwa neno hilo lenye kututakasa. Vilevile muziki unaelezwa kabla ya sanaa nyingine
kwa sababu unaambatana na maneno matakatifu. Mtaguso umesisitiza umuhimu wa kuimba katika
liturujia, ukiagiza malezi kwa ajili hiyo, uundaji wa kwaya, utungaji wa nyimbo ambazo zichote hasa
katika vitabu vya Biblia na liturujia. Kuhusu aina za muziki mtaguso umekubali aina yoyote inayoweza
kulingana na utakatifu wa ibada; vilevile umeruhusu ala mbalimbali za kufaa. Hata hivyo liturujia ya
Roma inapendelea muziki wa Kigregori na kinanda cha mabomba. Sanaa nyingine pia zinaheshimiwa
Page 10 of 21


11
na kutumiwa na Kanisa kwa ujenzi, mapambo, vifaa na picha takatifu. Kadiri ya mahali na nyakati
limekubali mitindo mbalimbali mradi ilingane na imani, maadili na ibada ya Kikristo. Mtaguso umeagiza
maaskofu hasa wajitahidi kudumisha msimamo huo na uzuri wa yote yanayohusu liturujia, kwa
kuelimisha wanasanaa na wakleri.

LUMEN GENTIUM

Hati hii juu ya Kanisa ndiyo muhimu kuliko nyingine zote. Inajibu swali la Paulo VI, “Kanisa,
unasemaje juu yako?”.
Sura ya kwanza inafafanua fumbo la Kanisa ambalo, kama sakramenti, lina mawili yasiyotenganika:
kwa nje linaonekana kwa namna fulani, na kwa ndani mwa neema ambayo haionekani ila inaletwa na
yale yanayoonekana. Ndani ya Kanisa la watu Mungu anaishi na kufanya kazi. Kwa hiyo hati inaanza
kwa kueleza jinsi Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanavyohusika na Kanisa. Halafu unaonyesha kuwa
Kanisa ni mwanzo wa ufalme wa Mungu, nalo linafananishwa na kundi la kondoo, shamba, jengo na
hekalu la Mungu au bibiarusi anayeungana na Bwanaarusi wake kuwa mwili mmoja, yaani mwili wa
Kristo: ndio ukweli wenyewe wa Kanisa.
Baada ya kuona ukweli huo wa ndani, sura ya pili inatazama jinsi watu wanavyohusika na fumbo la
Kanisa. Kuanzia Agano la Kale Mungu hakupenda kuwaokoa mmojammoja bali aliwaunganisha wawe
taifa lake lenye kujua ukweli na kumtumikia kitakatifu. Katika taifa hilo wote wamejaliwa ukuhani
unaotumika kuadhimisha sakramenti, na unabii wenye karama mbalimbali.
Katika taifa hilo watu wote wanapaswa kuingia bila ubaguzi ili wawe kitu kimoja. Ndiyo maana ya
jina “Katoliki”: la mahali pote na nyakati zote. Wote wanahusiana na Kanisa ila kwa namna mbalimbali.
Kwanza wapo Wakatoliki, yaani waliojiunga nalo kikamilifu kwa kumkubali Roho Mtakatifu na miundo
yake yote. Halafu wapo Wakristo wengine ambao wamebatizwa na hivyo wameungana nalo ingawa si
kikamilifu, kwa sababu hawakubali baadhi ya mafundisho na miundo yake. Hatimaye wapo watu
wengine pia, wenye dini mbalimbali au wasio na dini, ambao wote wanaitwa na Mungu wajiunge na
Kanisa kwa kuwa linahitajika kwa wokovu, ingawa yeye anaweza kuwaokoa wenye nia njema
wasiopata habari njema. Bila shaka hali ya Wakatoliki ni bora zaidi, nao wanapaswa kuwashirikisha
wengine wote ili kuwaokoa kutoka udanganyifu wa shetani na ulimwengu. Ndiyo maana ya umisionari
ambao umeagizwa na Yesu na ni wajibu wa kila Mkristo.
Sura ya tatu inatoa mafundisho muhimu tena mapya juu ya muundo wa uongozi wa Kanisa, hasa
uaskofu. Ni kwamba Mtaguso I wa Vatikano ulifundisha sana kuhusu Papa lakini haukupata nafasi ya
kutoa hati iliyopangwa juu ya maaskofu, kwa sababu ulisambaratika jeshi la Italia lilipoteka Roma.
Hivyo Mtaguso II wa Vatikano ulikusudia kukamilisha kazi hiyo.
Hasa umefundisha kwamba kama vile mitume walivyokuwa kundi moja na Petro na chini yake,
maaskofu wote ni kundi moja na Papa wa Roma na chini yake. Kwa mpango wa Mungu kundi hilo ni la
kudumu, maaskofu wakiwa waandamizi halisi wa mitume, na Papa mwandamizi halisi wa Petro, mkuu
wao.
Kwa namna ya pekee mtaguso umefundisha kuwa ibada ya kumweka wakfu askofu ni ngazi ya juu
kabisa ya sakramenti ya daraja, si baraka fulani kwa padri anayepewa kazi ya juu kama wengine
walivyodhani awali. Hivyo uaskofu unatia alama isiyofutika milele. Kutokana na fundisho hilo, mtaguso
umesisitiza kila mara umuhimu wa maaskofu katika maisha yote ya Kanisa.
Lakini mtaguso umesisitiza pia umoja wa maaskofu, ukidai kila mmojawao afanye kazi yake
akishirikiana na kundi lote na achangie ustawi wa Kanisa zima, si jimbo lake tu. Katika hilo askofu
ndiye nguzo ya umoja wa waamini wake wao kwa wao tena kati yao na waamini wote duniani: hivyo
anafanya listahili kuitwa Kanisa, kwa kuwa ndani ya jimbo Kanisa lote limo kweli. Kwa msingi huo
askofu anawakilisha Kanisa lake maalumu katika Kanisa Katoliki, na kulifundisha, kulitakasa na
kuliongoza kwa msaada wa mapadri wake na wa mashemasi, ambao wote wanashiriki ukuhani wake
mkuu.
Mwishoni mwa sura hiyo Kanisa la magharibi linaruhusu ushemasi wa kudumu urudishwe na
kutolewa kwa wanaume wenye ndoa pia.
Mara baada ya sura inayohusu wale wachache waliopata daraja takatifu (wanaoitwa wakleri),
inafuata sura ya nne juu ya Wakristo wa kawaida (wanaoitwa walei). Kwa karne nyingi hao walibaki
kama wasikilizaji na watazamaji tu katika ibada na katika maisha yote ya Kanisa, lakini katika karne
XIX utume wao ulianza kuamka upya. Mtaguso umesisitiza kwa nguvu wajibu na haki yao ya kutumia
neema na vipaji walivyojaliwa na Mungu kwa ujenzi wa taifa lake na kwa wokovu wa ulimwengu.
Msingi wake ni ubatizo uliowafanya manabii, makuhani na wafalme; hivyo wamejaliwa huduma na
karama mbalimbali ambazo wachungaji wanapaswa kuziheshimu wakiwaachia uhuru na nafasi katika
utendaji. Kwa namna ya pekee ni juu yao kulenga utawala wa Mungu kwa kushughulikia malimwengu.
Baada ya kuona hayo makundi mawili ya waamini, wanaotofautiana kwa alama walizotiwa rohoni na
sakramenti zisizorudiwa (ubatizo na kipaimara tu, au daraja takatifu pia), sura ya tano inazungumzia
wito unaowaunganisha wote, yaani kupata utakatifu. Karne za nyuma wengi walidhani hiyo ni kazi ya
Page 11 of 21


12
watawa tu, waliojichagulia “hali ya ukamilifu”, au sanasana mapadri. Kumbe sivyo: Wakristo wote
wanapaswa kulenga utakatifu, kila mmoja kadiri ya wito wake maalumu na hali yake maishani. Hati
inaorodhesha aina mbalimbali za waamini na kuonyesha jinsi kila moja ilivyo na njia yake; halafu
inakumbusha njia mbili bora, yaani kifodini na mashauri ya Kiinjili: kwa maisha na kifo chao watawa na
mashahidi wanahimiza Wakristo wote kutafuta ukamilifu wa upendo.
Hivyo ni rahisi kuelewa kwa nini sura ya sita inazungumzia watawa. Hao hawahusiki na uongozi wa
Kanisa (isipokuwa kama wamepata daraja takatifu), ila wanahusika moja kwa moja na utakatifu na
uhai wake. Si kundi la tatu kati ya wakleri na walei, bali ni walei au wakleri waliojifunga kulenga
utakatifu kwa kushika mashauri ya Kiinjili, yaani useja mtakatifu, ufukara na utiifu. Mtaguso
umesisitiza umuhimu wa mtindo huo wa maisha na asili yake katika maneno na mifano ya Yesu: utawa
hautokani na historia ya Kanisa tu, bali upo na lazima uwepo kwa mpango wa Mungu. Hivyo uongozi
wa Kanisa unapaswa kuuratibu na kuudumisha katika mitindo yake mingi. Mtawa amewekwa wakfu
kwa ubatizo, halafu anaimarisha hali hiyo kwa nadhiri ili achume kwa wingi zaidi matunda ya neema
kwa kuondoa mapingamizi yoyote yanayoweza kumzuia maishani.
Baada ya kuwafikiria watawa, wanaoshuhudia kwa namna ya pekee ulimwengu mpya ambako
hakuna ndoa, sura ya saba inakuja kufundisha kuwa Kanisa lote duniani liko safarini kuelekea
mbinguni, huku likiwa na umoja na watakatifu. Sura hiyo inasisitiza imani yetu kuhusu mambo ya
mwisho ikituhimiza tutazame juu na pia tuzingatie mifano bora ya wale waliokwishafikia heri ya milele.
Hao wanastahili tuwaheshimu na kuwaomba watuombee, mradi tuepuke makosa mbalimbali
yaliyojitokeza huku na huku. Daima ionekane wazi kuwa tunamuabudu Mungu tu na kwamba
tukiwaheshimu watakatifu ni kwa sababu ni marafiki wa Mungu na wafuasi hodari wa Mwanae.
Tusiwaheshimu tu ili kupata msaada fulani, bali hasa kwa kufuata mifano yao ili tuwafikie katika
liturujia ya mbinguni kuwaabudu Mungu na Mwanakondoo.
Mwishoni mwa hati hii yanapatikana mafundisho kuhusu Bikira Maria, akiwa mkuu wa watakatifu na
mfano wa Kanisa lote. Baada ya mabishano makali kati ya washiriki wa mtaguso, wingi wa kura
ulikataa kutoa hati maalumu juu ya Maria peke yake, kwa kuwa hawezi kueleweka nje ya fumbo la
Kristo na la Kanisa. Hivyo mafundisho hayo yameingizwa katika hati hii kama sura ya nane, si kwa nia
ya kuamua mabishano kati ya wanateolojia, wala kufundisha mapya, bali kupanga upya mafundisho ya
Maandiko na ya Mapokeo. Baada ya kumsifu sana Bikira, mtaguso umesisitiza juu yake pia kuwa Kristo
ndiye mshenga pekee kati ya Mungu na watu, hivyo hatuwezi kumlinganisha Maria na yeye kama
walivyowahi kufanya baadhi ya waamini. Mchango wake kwa ukombozi wetu ulitokana na ukombozi
ulioletwa na Yesu, ni kushiriki kazi yake tu. Hivyo Maria azidi kuigwa na kuheshimiwa kwa namna ya
pekee, hasa kwa njia ya liturujia, lakini kwa kukwepa neno lolote ambalo linapita kiasi au kumweka
pembeni Kristo.
Wazo kuu la hati hii kuhusu Kanisa ni kwamba lenyewe hasa ni ushirika wa Mungu nafsi tatu na
watu, ni ushirika wa watakatifu wa duniani, toharani na mbinguni, ni ushirika wa waamini wa aina
mbalimbali, kama vile wenye daraja na walei, au watawa na wenzao wote. Ushirika huo unatakiwa
kuonekana wazi maishani mwa Kanisa katika ngazi zote; hivyo litaonekana lilivyo, yaani ishara na
chombo cha kuwaunganisha watu wote katika umoja wa Utatu mtakatifu.

DEI VERBUM

Tangu zamani sana Kanisa Katoliki lilisisitiza liturujia na sakramenti, ingawa lugha ya kawaida
ilikuwa haitumiki katika ibada hizo. Hivyo waamini walikuwa hawaelewi masomo ya Biblia wala matini
mengine. Kwa jumla walikuwa hawaelewi Neno la Mungu kwa kukosa tafsiri za vitabu vyake hata
nyumbani. Kuanzia karne XII tafsiri hizo zilianza kupatikana kwa juhudi za wazushi waliozitumia
kupinga Ualimu wa Kanisa. Watu walipobuni uchapishaji huko Ujerumani, Biblia ikawa kitabu cha
kwanza kutolewa. Miaka michache baadaye ukaanza Uprotestanti ambao katika madhehebu yake yote
ulisisitiza Maandiko kwa kukataa Mapokeo na Ualimu wa Kanisa. Ndiyo sababu ulifanya kazi kubwa ya
kutafsiri na kueneza Biblia ulimwenguni kote. Upande wake Kanisa Katoliki liliogopa kwa kuona nchi
ngapi zimeliasi, hivyo likachukua msimamo wa kinyume kwa kusisitiza tena Mapokeo na Ualimu wake.
Basi, Biblia ikazidi kubaki pembeni mwa maisha ya Wakatoliki wengi. Hata mwanzoni mwa karne XX
wataalamu walikatazwa wasifundishe baadhi ya mambo mapya juu ya Maandiko. Hivyo kabla ya
mtaguso Wakatoliki kwa jumla walikuwa wakiogopa Biblia badala ya kuipenda.
Kumbe hati hii kuhusu ufunuo wa Kimungu ilipotolewa baada ya majadiliano na marekebisho mengi
imelirudishia Kanisa lote Maandiko Matakatifu. Hapo Wakatoliki wataalamu wa Biblia wamefanya kazi
kubwa sawa na wenzao Waprotestanti. Waseminari na watawa wengi wamefundishwa sana Neno la
Mungu, na hata walei wameanza kulifurahia. Matunda yake yamepatikana tayari katika uzima mpya
unaoonekana katika matapo ya Kiroho, vyama na jumuia mbalimbali.
Baada ya dibaji, inayotamka nia ya kufuata nyayo za mitaguso iliyotangulia, sura ya kwanza
inazungumzia ufunuo wa Mungu. Ni kwamba hatuwezi kuelewa Biblia mbali na historia ya wokovu, kwa
Page 12 of 21


13
sababu si kitabu kilichoandikwa leo kwa ajili yangu mimi, bali kilipatikana zamani Mungu alipojifunua
hatua kwa hatua hadi ulipokamilika wakati wa Yesu.
Sura ya pili inafundisha ufunuo huo unavyotufikia sisi, watu wa leo, kwa njia ya Mapokeo ya Mitume
yakiwa na Maandiko Matakatifu: hayo si chemchemi mbili tofauti bali kwa pamoja ni hazina ya Neno la
Mungu. Hazina hiyo imekabidhiwa kwa Kanisa ambalo linaweza kuifafanua rasmi kwa njia ya Ualimu
wake. Basi, Mapokeo Matakatifu, Maandiko Matakatifu na Ualimu wa Kanisa vimeshikamana na
kuunganika kiasi kwamba kimoja hakiwezi kusimama bila vingine.
Baada tu ya kuelewa hayo tunaweza kukabili Biblia yenyewe (sura ya tatu inavyofanya) kwa
kuzingatia jinsi Roho Mtakatifu alivyovuviwa juu ya waandishi wake. Hao walifanya kazi kama
waandishi wowote, lakini vitabu vilivyopatikana vinafundisha tu kwa hakika na bila kosa ule ukweli
ambao Mungu alitaka uandikwe kwa wokovu wetu. Si ukweli wowote (k.mf. kuhusu sayansi) bali ule
unaohusu wokovu. Hivyo Biblia, mwandishi wake hasa ni Mungu, lakini yeye alijieleza kwa njia ya
watu, tena kwa namna ya kibinadamu. Basi, tukitaka kumuelewa tunapaswa kuelewa kwanza
waandishi walitaka kusema nini, tukizingatia pia mitindo waliyoitumia. Utaalamu huo ni muhimu
ingawa hautoshi, kwa sababu tunapaswa bado kuzingatia Biblia nzima, Mapokeo ya Kanisa na kweli za
imani.
Baada ya kuona habari za Biblia kwa jumla, sura ya nne inaeleza Agano la Kale lilivyo muhimu kwa
Wakristo pia, kwa kuwa linashikamana na Agano Jipya kama kitabu kimoja ambacho pande zake mbili
zinahitajiana.
Sura ya tano inaeleza juu ya Agano Jipya: kwanza ubora wake unaozidi vitabu vya kale; halafu asili
ya Kitume ya Injili nne ambazo tena zinapita hata Maandiko mengine ya Agano Jipya; mwishowe
hakika ya kihistoria ya Injili hizo. Hati hii imepokea pia mtazamo mpya uliosema Wainjili waliandika
historia ya Yesu kwa kuchagua, kufupisha na kueleza upya habari kadiri ya mazingira, wakidumisha
namna ya kuhubiri kwa lengo la kufanya watu waamini. Habari zenyewe ziliwaelea kwa mwanga wa
Roho Mtakatifu aliyelifikia Kanisa baada ya Kristo kufufuka ili kuliongoza kwenye ukweli wote.
Hatimaye sura ya sita inatoa maagizo kuhusu Maandiko Matakatifu katika maisha ya Kanisa.
Kwanza ziwepo juhudi mpya ili wote wapate lishe katika meza ya Neno la Mungu ambalo ni hai na lina
nguvu. Waamini wapate Maandiko hayo katika lugha zao. Wataalamu pamoja na kuyatafsiri
wayafafanue na kuelimisha wengine. Wale wote wanaofundisha imani washikamane na Maandiko kwa
kuyasoma pamoja na kusali ili Biblia iwe kiini cha mafundisho yao. Waamini wote, hasa watawa,
waisome sana kwa sababu kutoijua ni sawa na kutomfahamu Kristo.

GAUDIUM ET SPES

Hati hii, ndefu kuliko zote, inaitwa ya kichungaji kwa sababu inatazama mambo kwa lengo la
kuongoza maisha ya watu. Kichwa kinasema wazi kuwa hati inahusu Kanisa katika ulimwengu “wa
kisasa”, kwa kuwa tunapaswa daima kuishi na kutenda “leo”, huku tukijua vizuri mambo yalivyo,
tukitambua ishara za nyakati zijazo ili tuone njia za kufaa kwa wokovu wa ulimwengu. Sehemu ya
kwanza inaweka misingi ya imani, na sehemu ya pili inatoa msimamo wa Kanisa kuhusu ulimwengu wa
leo.
Kanisa halijioni tena mbali na ulimwengu, wala dhidi ya ulimwengu, bali ndani ya ulimwengu.
Wakristo wanasafiri duniani pamoja na binadamu wenzao, wakishirikiana nao katika yale yote
yasiyopingana na imani na maadili ya Kikristo. Hasa walei, ambao idadi yao ni karibu sawa na idadi ya
wanakanisa wote, wanapaswa kuishi ulimwenguni kama chachu mpaka donge lote liumuke. Basi,
Kanisa linajisikia kuhusika kabisa na maisha ya watu wote, hasa mafukara. Ndiyo maana maneno ya
kwanza ya hati hii yanasema kuwa “furaha na matumaini, huzuni na mafadhaiko ya watu ni pia ya
wanafunzi ya Kristo”.
Hati hii, iliyo ujumbe wa Kanisa kwa wote, unakusudiwa kuwasaidia waelewe mambo yanayotukia
waweze kujipatia maisha bora kweli na halafu uzima wa milele; la sivyo watadanganyika na kupotoka.
Leo kuna ugumu wa pekee kwa kuwa mabadiliko ya kila aina yanatokea haraka ajabu. Mtu wa kawaida
hapati nafasi ya kuyafikiria kwa dhati na kuyachambua ili kujifanyia mpango wa kumfaa. Hivyo hatari
yake ni kufuata mkondo au kuongozwa na matukio, hata akafikia hatua ya kushindwa kujielewa ni
nani, pamoja na kukosa msimamo maishani na raha moyoni. Basi, anahitaji kuelekezwa kwa imani na
upendo: ndiyo kazi ya Kanisa ambalo lina nafasi nzuri ya kuwatangazia watu majibu ya Injili kwa
maswali yanayowakera.
Kwa ajili hiyo hati inamuongoza msomaji hatua kwa hatua kufikiria utatanishi wa kisasa katika
nadharia, jamii, uchumi na siasa unaomfanya afadhaike, hasa akiona maendeleo hayafaidishi wote na
pengine yanatumika dhidi ya binadamu. Basi, atambue kuwa shida zinaanza moyoni mwake, ambamo
mna mashindano makali na maswali ya msingi kama vile, “Mtu ni nani? Mateso na kifo, vinavyodumu
hata wakati huu wa maendeleo makubwa, maana yake nini? Mtu ailetee nini jamii na atarajie kupata
nini toka kwake? Baada ya maisha haya kutakuwa na nini?”. Jibu ni Kristo, mwokozi pekee, kiini na
lengo la historia yote, msingi usiobadilika. Katika mwanga wake mtaguso umechunguza fumbo la
binadamu na wito wake.
Tangu hati iandikwe, imepita miaka mingi, hivyo yameshatokea mabadiliko mengi, yaliyochunguzwa
na mapapa na sinodi mbalimbali. Leo baadhi ya mambo ni tofauti kidogo, hata hivyo hati inabaki
muhimu: kwanza kwa mtazamo wake wa jumla, pili kwa mtindo wa kuwaelekeza watu katika mambo
Page 13 of 21


14
ya kawaida yanayowahusu maishani, tatu kwa mafundisho ya msingi yasiyoweza kubadilika, nne kwa
kuwa misimamo mingi inafaa mpaka leo.
Katika sehemu ya kwanza, sura ya kwanza inaeleza hadhi ya binadamu yeyote. Ingawa karibu wote
wanakubali kuwa mtu ni kiumbe bora duniani, Kanisa linasisitiza ukweli huo kwa kumuona na kumuita
“sura ya Mungu” hata baada ya kuathiriwa na dhambi. Ndio msingi wa heshima anayostahili katika
mwili na zaidi katika roho ambayo kwa akili inaweza kujipatia ukweli na hekima, kwa dhamiri inasikia
wito wa Mungu, na kwa hiari inaweza kuuitikia. Lakini Kanisa, pamoja na kusisitiza hiari kama
wanavyofanya wengi siku hizi, linahimiza pia kuitumia vizuri, na linakumbusha kuwa mwishoni kila mtu
atahukumiwa juu ya matumizi ya vipawa vyake.
Baada ya kukabili suala la kifo kwa kutangaza habari njema ya ufufuko, hati inakabili janga
mojawapo la siku hizi, yaani kwamba wengi wanakanusha uwepo wa Mungu au wanaishi bila kumjali.
Mtaguso ulifikiria hasa ukomunisti na misimamo mingine ya kupinga na kuzuia dini zote, lakini badala
ya kuilaani tu, umetuhimiza kujadiliana na kushirikiana nayo, pamoja na kutoa ushuhuda wa maisha
bora ya Kikristo, ukikiri kuwa pengine mifano yetu mibaya ndiyo iliyosababisha wengi wakose imani.
Mwisho unachora taswira ya Kristo, mtu mpya, ambaye peke yake anaangaza fumbo la binadamu
pamoja na uchungu na kifo.
Sura ya pili inatoa mafundisho kuhusu jamii yanayozingatia mpango wa Mungu wa kuwa watu
waishi kwa ushirikiano. Kuukamilisha ushirikiano huo kwa msingi wa haki ni muhimu kuliko maendeleo
ya ufundi tu. Kwa ajili hiyo kila mtu awajibike kuhusu wenzake wote bila kumsahau hata mmoja,
akijifanya jirani wa wenye shida na kujitahidi kustawisha usawa kwa kutumia nafasi yoyote aliyonayo
katika jamii. Maadili ya kibinafsi hayakubaliki, bali wajibu mkuu mmojawapo ni kujihusisha na ustawi
wa jamii na mshikamano ili wote kwa neema ya Kristo waishi kijamaa.
Sura ya tatu inatoa msimamo kuhusu utendaji wa binadamu. Hasa leo ambapo maendeleo ni ya
haraka tunajiuliza kuhusu maana ya juhudi zetu na namna ya kuziendeleza. Ni hakika kuwa Mungu
ametuagiza tufanye kazi na kutawala ulimwengu ili wote wapate hali ya maisha wanayostahili walio
sura yake. Wakristo wanapaswa kuwa mstari wa mbele bila kudhani eti, Mungu anauonea kijicho
ushindi wowote wa binadamu juu ya maadui wake (ujinga, maradhi na ufukara). Kumbe ushindi huo
unatangaza ukuu wa Mungu aliyemuumba mtu akiwa na akili nyingi.
Lakini binadamu asisahau kuwa ubora wake hautegemei wingi wa vitu anavyojipatia, bali tunu za
kiadili anazostawisha kwa kazi yake, hasa haki na udugu. Kumbe mara nyingi anafuata ubinafsi au
utaifa na kuanzisha miundo ya dhuluma na vita hata kutengeneza silaha zinazotosha kuangamiza uhai
wowote duniani. Mbele ya hali hiyo sisi Wakristo tusifuate mitindo ya ulimwengu bali njia ya upendo
nyuma ya Kristo, tukiwa tayari kubeba msalaba wanaotwishwa wale wanaotafuta haki na amani.
Tumaini la uzima wa milele lisipunguze bidii yetu kwa maisha ya binadamu wa leo, kwa kuwa huyo
anaandaliwa hapa duniani kuingia katika ufalme wa mbinguni.
Katika utendaji ni haki kufuata taratibu za elimudunia , siasa n.k. Imani haiogopi kumuachia mtu
nafasi hiyo, kwa kuwa Mungu yuleyule aliyejifunua kwetu kwa imani ameumba pia vitu vyote na
kutujalia akili na uvumbuzi. Mtaguso umelaumu mawazo finyu yanayogonganisha imani na sayansi.
Kutokana na zile zilizotangulia, sura ya nne inaeleza uhusiano wa Kanisa na ulimwengu. Kanisa
lengo lake ni la milele, lakini linaishi duniani na wanae pia ni raia wa nchi fulani. Kwa hiyo, ingawa
utume wake ni wa kidini hasa, linashughulikia pia ustawi wa jamii na umoja wa mataifa. Pamoja na
kupokea kwa shukrani misaada mbalimbali ya walimwengu, lina ujumbe kwa watu wote kuhusu
wokovu, tena kuhusu maisha haya, hasa hadhi na haki za kila mmoja. Wakristo wasirudie kusahau
majukumu ya kidunia, wala wasiyaone hayahusiki na imani. Kati ya makwazo makubwa ya nyakati
zetu, mojawapo ni utengano wa imani na maisha ya Wakristo wengi. Kwa mfano wa Yesu huko
Nazareti, walei wanapaswa kushughulikia malimwengu yote, wasisubiri kuagizwa na wachungaji wao,
kwa kuwa kuratibu hayo ni kazi yao hasa. Mtaguso ukikiri tena ukosefu wa wanakanisa umewahimiza
kujirekebisha wasije wakazuia uenezaji wa Injili. Vilevile umesifu juhudi za watu wowote kwa
kustawisha familia, utamaduni, uchumi, jamii, amani na mshikamano wa kimataifa, hata ukasema
Kanisa limefaidika sana na upinzani na dhuluma za maadui wake.
Kisha kueleza kwa jumla jinsi Kanisa linavyohusika na wito wa binadamu, hati hii katika sehemu ya
pili inakabili masuala kadhaa yaliyo muhimu zaidi kwa watu wa leo.
Sura ya kwanza inafafanua hadhi ya ndoa na familia na namna ya kuzipa nafasi za kufaa, kwa
sababu mengine mengi yanategemea hali ya familia. Baada ya kueleza utakatifu wa ndoa, kwa
kuifananisha na hali ya kuwekwa wakfu kwa njia ya sakramenti za kudumu, mtaguso umeonyesha
ubora wa upendo kati ya mume na mke na namna ya kuutekeleza, ukisisitiza unavyoelekea uzazi.
Hivyo watu wa ndoa waupange kwa pamoja mbele ya Mungu na kwa kuzingatia mafundisho ya Kanisa
ili wazae kwa busara na ukarimu. Kwa namna ya pekee ni lazima uhai wa binadamu kisha kuanza
ulindwe kwa bidii zote: kuua mimba au mtoto ni maovu ya kutisha. Katika magumu yanayohusu uzazi
wa mpango, wanandoa wajitahidi kufuata namna ya usafi wa moyo inayowafaa. Jamii nzima inatakiwa
Page 14 of 21


15
kuchangia ustawi wa familia: viongozi watunge sheria na kufanya mipango kwa ajili hiyo; wanasayansi
waendelee kutafuta njia halali za kupanga uzazi; mapadri wafanye juu chini familia ziishe kwa utulivu.
Sura ya pili inakusudia kustawisha utamaduni, yaani namna maalumu ambazo binadamu anakabili
maisha katika mazingira na nyakati mbalimbali ili kujiendeleza kulingana na orodha ya tunu
anazothamini. Tofauti na wanyama, yeye hawezi kufikia maisha ya kumfaa kweli asipoyafanyia kazi
mema yaliyoumbwa na Mungu ndani mwake na kandokando yake. Kila kabila na kundi la watu lina
utajiri wake. Lakini huu wa leo ni wakati mpya wa historia. Upande mmoja zimefunguliwa njia mpya za
kukuza na kueneza elimu na za kuunganisha aina tofauti za utamaduni. Upande mwingine kuna hatari
za kufuta hekima na sura maalumu za jamii tofauti, kuvuruga mafungamano kati ya vizazi, kuacha
elimu ya juu mikononi mwa wataalamu tu n.k.
Amri ya upendo inadai Wakristo wachangie na wenzao ujenzi wa ulimwengu ili wote waone vizuri
kazi ya Mungu na namna ya kuiendeleza. Kama vile yeye alivyotumia utamaduni wa watu ajifunue
kwao, ndivyo Kanisa pia lilivyofanya na linavyopaswa kufanya katika kueneza habari njema. Kwa kuwa
limetumwa kwa mataifa yote, halibanwi na utamaduni wowote, bali linautumia na kuuchangia,
linausafisha na kuuinua lisiishie ndani yake. Ni wajibu wa wote kufuta ujinga kwa kueneza elimu hasa
ya msingi ili kila mtu aweze kuchangia zaidi ustawi wa jamii. Vilevile kila mmoja aelewe wajibu wa
kujiendeleza kiutu na Kiroho, akitumia vitabu na vyombo vingine vya upashanaji habari, muda huru
alio nao n.k. asitawaliwe na kazi za mikono tu.
Sura ya tatu inafundisha kuhusu maisha ya kiuchumi na ya kijamii ya mtu wa nyakati zetu. Ni
lazima huyo awekwe juu kabisa kuliko maendeleo ya vitu, kwa kuwa ndiye mtendaji, kiini na lengo la
uchumi na la jamii. Kumbe wengi wanazingatia sheria za uchumi tu ili kutajirika iwezekanavyo.
Matokeo ni kwamba mtengo kati ya mataifa, na kati ya matabaka ndani ya nchi, unazidi kuwa
mkubwa. Anasa za wachache zinaleta ufukara wa kutisha wa umati hata kuhatarisha amani duniani.
Binadamu anaweza kurekebisha hali hiyo, lakini yanahitajika mageuzi mengi katika mitazamo,
mazoea na miundo pia. Hapo tu ongezeko la uzalishaji litasaidia kweli, yaani litamsaidia mtu yeyote
katika mahitaji yake yote (ya mwili, ya nafsi na ya roho). Kwa ajili hiyo ni lazima uchumi usiachwe
uende zake wala usitawaliwe na wachache, bali wote waweze kuchangia ustawi na uongozi wake bila
ubaguzi, wakisaidiwa kushika nafasi yao hasa kwa njia ya ustadi. Kazi ya binadamu iheshimiwe kuliko
mengine yanayohusu uchumi (k.mf. mtaji au malighafi). Wote wana wajibu na haki ya kufanya kazi na
kujipatia hivyo riziki za kutosha. Vilevile wana haki ya kupata muda kwa maisha ya kifamilia, hasa
akina mama. Wafanyakazi ni haki yao kuchangia uongozi wa kampuni, na vilevile kuunda vyama vya
kutetea haki zao hata kwa migomo.
Mojawapo kati ya mambo yaliyozingatiwa zaidi na mtaguso ni njaa ya umati; kwa ajili hiyo
umekumbusha kuwa Mungu ameumba vyote kwa ajili ya wote, basi ni lazima mali zigawiwe kwa haki
na upendo. Ingawa mtu yeyote ana haki ya kumiliki vitu kadhaa, ni lazima kila mmoja awe na mali za
kutosha, wasiwepo wanaojipatia mali nyingi kiasi cha kuacha wengine wakose hata mahitaji. Matajiri
wawajibike haraka kuwashirikisha wengine, la sivyo watakuwa wauaji wa wenye njaa. Hao wa mwisho
ni haki yao kujipatia riziki kutoka utajiri wa wenzao. Kadiri ya mazingira zinaweza kuwepo njia tofauti
za kuhakikisha wote wapate riziki zao (desturi za ukarimu, pensheni n.k.). Mashamba yagawiwe kwa
wakulima wasiyonayo. Pesa zitumike kuandaa nafasi za kazi kwa watu wa leo na wa kesho wa nchi
zote (vitegauchumi). Wakristo walenge ufalme wa Mungu hata katika uchumi na shughuli nyingine za
kijamii.
Sura ya nne inafikiria siasa ambayo pia siku hizi inapitia mageuzi makubwa. Mchango wa Kanisa ni
kutetea heshima ya kila mtu kwa kusisitiza kwamba lengo la siasa ni ustawi wa jamii nzima kuanzia
watu na familia. Wananchi wote waelimishwe kuhusu siasa ili watoe mchango wao kwa kutumia nafasi
wanazopewa (kura n.k.) na kwa kutetea haki zao bila kuwadai mno viongozi. Hao wanahitajika ili
kulinganisha kwa haki madai ya watu mbalimbali. Jamii na Kanisa vinahudumia kwa namna tofauti
watu walewale, hivyo ni vema vishirikiane bila kuchanganyikana. Kanisa halifungamani na siasa
yoyote, liwe huru kutangaza maadili yanayotakiwa hata katika siasa, likipima mambo yote na kuhimiza
yaliyo mema.
Hatimaye, sura ya tano inaongelea ujenzi wa amani na umoja kati ya mataifa. Wakati ilipoandikwa
ulikuwa wa hofu kubwa kuhusu dunia nzima kuja kuangamizwa na wingi na ukali wa silaha
zilizotengenezwa. Kwa msingi huo suala la vita lilitakiwa kufikiriwa upya, bila kuridhika na msimamo
wa zamani kuhusu masharti ya uhalali wake. Wakristo wa madhehebu yoyote tuungane kati yetu, tena
na wote wenye mapenzi mema, katika kujenga amani na haki. Amani ya kweli si tu kusimama kwa
vita, labda kwa kuogopa tu silaha zilizorundikana; bali ni tunda la haki ambayo itafutwe mfululizo kwa
bidii, tena ni tunda la upendo ule wenye msingi ndani ya Mungu. Kuhusu vita vinavyoendelea huku na
huku, kwanza ukatili wake upunguzwe (kumbe siku hizi umezidi kwa sababu ya silaha mpya,
mashambulizi ya raia, maangamizi ya kabila zima n.k.). Magizo hayawezi kuwa kisingizio cha kutenda
maovu, bali ni wajibu kuyakataa. Mapatano ya kimataifa kuhusu vita yaheshimiwe na wote. Ni wajibu
wa viongozi wa nchi kuilinda hata kijeshi, lakini wasitumie jeshi kugandamiza wengine. Pia waheshimu
dhamiri ya wasiojisikia kutumia silaha. Vitendo vinavyowezekana leo vya kuangamiza maeneo mapana
Page 15 of 21


16
na wote waliopo ni makosa ya jinai yasiyovumilika. Wanaotengeneza au kununua silaha ili kujikinga na
maadui wasije wakashambuliwa, wafikirie hatari ya silaha hizo kuja kutumika kweli, tena hasara ya
maskini wanaokosa misaada wanayostahili kwa sababu tu pesa nyingi sana zinatumika kwa silaha.
Tutafute mapema njia za upatanisho na muundo wa kimataifa wenye uwezo wa kudumisha amani na
haki kwa wote. Hapo katikati akiba za silaha zipunguzwe kwa mpango wa pamoja. Viongozi na watu
wao waache utaifa na misimamo yoyote inayotenganisha watu. Hasa malezi ya vijana na upashanaji
habari vieneze mawazo ya amani na mitazamo mipana yenye faida kwa wote. La sivyo tutafikia tu ile
amani ya kutisha itakayopatikana kwa kufa sote. Kanisa likisema hivi haliachi kutumaini na kuhimiza
wongofu wa mioyo.
Kuhusu kuunganisha mataifa, mara nyingi misingi ya kutoelewana ni hali za uchumi tofauti mno,
nia ya kutawala, dharau ya wengine na vilema mbalimbali. Basi, ushirikiano mkubwa unaowezekana
leo ulenge kutatua matatizo hayo na kukidhi mahitaji ya watu, hasa maskini. Miundo ya kimataifa
iliyopo izingatie zaidi nchi zinazoendelea, wakimbizi na wengine wenye shida maalumu.
Ingawa miaka ile ya mtaguso nchi nyingi zilipata uhuru wa kisiasa, hali ya uchumi inazirudisha chini
ya ukoloni mpya. Basi, mshikamano uendeleze kweli nchi hizo. Lakini maendeleo yanategemea watu
kuliko pesa, kwa hiyo kazi ya kwanza ni kuandaa raia wa nchi maskini kwa elimu na ufundi.
Unahitajika ukarimu wa misaada, mikopo na vitegauchumi, lakini pia kurekebisha sana sheria za
uchumi wa kimataifa. Upande wao viongozi wa nchi maskini wapokee misaada kwa uaminifu, na raia
wao wajitahidi kutumia vile vyote walivyo navyo. Maendeleo ya uchumi yasisahaulishe roho ya
binadamu, kwa kuwa huyo haishi kwa mkate tu.
Wengi leo wanafadhaishwa na kasi ya ongezeko la watu. Utatuzi wa kwanza ni kuleta usawa
mkubwa zaidi kati ya watu na kueneza ujuzi kuhusu kilimo n.k. Halafu zitungwe sheria zinazosaidia
familia, izuiwe kasi ya watu kuhamia mijini, elimu itolewe kwa ukweli kuhusu hali ya nchi na uzazi wa
mpango. Wote wajiepushe na njia za mkato zinazokwenda kinyume cha maadili na cha haki ya msingi
ya wananchi kufunga ndoa na kuzaa wanavyoona vema wenyewe. Basi, wasaidiwe kuunda dhamiri na
kujifunza njia halali za kupanga uzazi.
Wakristo wawe mstari wa mbele katika mshikamano wa kimataifa, wakijua Yesu katika mafukara
analia na kudai upendo. Mtaguso uliita kikwazo kuona nchi za Kikristo zikitapanya mali, wakati
nyingine zinalemewa na njaa, maradhi n.k. Wakristo wajitolee kuhamia kwenye shida ili kusaidia kwa
hali na mali, wakishirikiana na miundo na watu wowote, kwa kuwa tunaye Baba mmoja na tunapaswa
kuishi sote kidugu. Hapo watatambulikana kama wafuasi halisi wa Kristo. Tukikumbuka kuwa
hatutaingia mbinguni kwa kusema tu, Bwana, Bwana, bali kwa kutimiza mapenzi ya Baba, tukabili kazi
hiyo kubwa ambayo siku ya mwisho tutahukumiwa kwa jinsi tulivyoifanya.

INTER MIRIFICA

Hati hii ilitolewa mapema ili kukabili jambo ambalo siku hizi ni zito sana kwa jinsi linavyochangia
maisha na utamaduni wa watu duniani kote, yaani vyombo vya upashanaji habari. Hivyo vimeendelea
hasa katika karne XX na kuwafikia karibu watu wote vikieneza habari, mawazo, maadili n.k. Kanisa
linavipokea kwa shukrani kwa Mungu aliyempa binadamu akili ya kuvumbua na kubuni njia hizo
zinazoweza kumuinua hata kidini. Lakini kwa ubaya wa moyo wake anaweza pia kuzitumia kwa
uharibifu wake na wa wengine wengi, hasa watoto na vijana wasio na kinga. Kwa hiyo Kanisa
linapaswa kushughulikia vyombo hivyo vyote vitumike vema kwa kueneza habari njema, maadili na
taarifa za kweli ili watu wakabili maisha vizuri na kuokoka. Pia liwaelimishe wote kuhusu namna ya
kuchuja na kutumia vilivyo magazeti, vitabu, filamu, redio, televisheni n.k., wakielewa urahisi wa
kudanganywa na kupotoshwa navyo. Hiyo ni kazi ya wachungaji, wazazi na walezi, lakini serikali pia
isaidie kutunza mazingira safi upande wa maadili. Mtaguso umeagiza shughuli hizo ziratibiwe kijimbo,
kitaifa hata kimataifa. Kwa kuwa zina gharama kubwa, Wakristo wanahimizwa kujitolea kwa ukarimu
hasa Jumapili maalumu moja kwa mwaka.

ORIENTALIUM ECCLESIARUM

Mtaguso ulizingatia hali duni ya Makanisa Katoliki ya mashariki ukaamua kuirekebisha. Kwanza
ulitamka kuwa yanastahili kuheshimiwa sana pamoja na mambo yake yote ya pekee (liturujia, teolojia,
sheria, miundo n.k.) kama sehemu ya hazina ya Kimungu iliyokabidhiwa kwa Kanisa. Liturujia hizo
zitunzwe kiaminifu na kurekebishwa kama zimeachana na mapokeo ya mashariki, hasa sakramenti
zirudi kufuata taratibu asili. Mashirika ya Kilatini yajitahidi kuanzisha jumuia za kimashariki.
Madhehebu yoyote ya Kikatoliki yana haki na wajibu sawa hata kuhusu uenezaji Injili duniani kote.
Maaskofu na mapadri wa mashariki na magharibi wazoee kushirikiana, na wanaojiandaa kupata upadri
waelimishwe juu ya uhusiano kati ya madhehebu hayo yote. Waamini wa mashariki wapatiwe mapadri
na hata maaskofu wao popote wanapohitaji. Waorthodoksi wakijiunga na Kanisa Katoliki waendelee
kufuata madhehebu yao, na wakiwa na daraja yoyote waendelee kuitumia. Kutokana na umuhimu wa
patriarki kwao, hadhi na haki zake zirudishwe kama zilivyokuwa kabla ya farakano, na Makanisa yasiyo
naye yafikiriwe. Hatimaye hati inahimiza Wakatoliki wa mashariki kushughulikia ekumeni hasa upande
wa Waorthodoksi, ikiruhusu kutoleana nao sakramenti kadhaa na mengineyo.
Page 16 of 21


17

UNITATIS REDINTEGRATIO

Kurudisha umoja kati ya Wakristo wote ni lengo kuu mojawapo la mtaguso. Mafarakano yaliyokata
mwili wa Kristo vipandevipande ni kinyume cha matakwa yake na yanakwaza ulimwengu usiamini.
Siku hizi Mungu ametuhurumia na kututia hamu ya umoja hata ukatokea mfumo wa ekumeni. Kwa
hati hii Kanisa Katoliki linawajibika kushirikiana na madhehebu yoyote ya Kikristo lisije likazuia kazi
hiyo ya Roho Mtakatifu.
Sura ya kwanza inaeleza msimamo wa Kikatoliki kuhusu ekumeni. Imani yetu ni kwamba Kanisa ni
moja tu, nalo limekabidhiwa kwa waandamizi wa mitume chini ya mwandamizi wa Petro. Tunakiri kuwa
mafarakano yaliyotokea yalisababishwa na makosa ya pande zote. Waliolelewa Kikristo nje ya Kanisa
Katoliki hawawezi kulaumiwa, tena ni Wakristo halisi na ndugu zetu, ingawa ushirika wetu si kamili.
Tuwaheshimu pamoja na mema yao mengi ambayo yanatokana na Mungu na kuelekea ujenzi wa
Kanisa. Makanisa yao au jumuia zao vinatumiwa na Mungu kama vyombo vya wokovu, ila katika
Kanisa Katoliki tu unapatikana ukweli mzima na vifaa vyote vya wokovu. Hata hivyo tunakiri kwamba
hatutumii vizuri neema hizo na hata tunawakwaza wenzetu; basi, tunapaswa kulenga ukamilifu wa
Kikristo ili Kanisa ling’ae mbele ya wote. Mbali ya matendo ya kupendana ni muhimu pia majadiliano
ya kiteolojia na mikutano ya sala ya pamoja.
Sura ya pili inaeleza utekelezaji ikisisitiza unavyowapasa waamini wote, kwa njia ya kurekebisha
Kanisa, kuongoka, kusali, kushirikishana sakramenti, kufahamiana, kueleza imani kwa usahihi na bila
kudharau madhehebu mengine, kushirikiana katika kutetea haki na amani na kuleta maendeleo.
Sura ya tatu inaeleza kifupi historia ya mafarakano kwa kutofautisha sana yanayohusu
Waorthodoksi na yanayohusu Waprotestanti, hasa kutokana na makundi hayo mawili kuwa au
kutokuwa na daraja halisi na hivyo kuwa au kutokuwa na ekaristi. Kwa msingi huo yanastahili kuitwa
Makanisa au jumuia za Kikanisa tu. Uhusiano wetu na makundi hayo ni tofauti, na uwezekano wa
kushirikiana katika sakramenti ni mkubwa kwa Waorthodoksi bali ni mdogo kwa Waprotestanti.
Mwishoni hati hii inakiri kuwa ekumeni inapita uwezo wetu, kwa hiyo tegemeo lote ni katika sala ya
Yesu kwa Kanisa, katika upendo wa Baba na katika uwezo wa Roho Mtakatifu.

CHRISTUS DOMINUS

Mtaguso, baada ya kufundisha wazi juu ya daraja ya maaskofu, ulitunga hati nyingine kuhusu
utendaji wao katika ngazi tatu: Kanisa zima, Makanisa maalumu na ujirani mwema wa majimbo.
Maagizo yote ya hati hii yalikusudiwa kuongoza marekebisho ya sheria za Kanisa.
Kwanza askofu yeyote ni kiungo cha kundi la maaskofu ambalo linaongozwa na askofu wa Roma
likiwajibika kulichunga Kanisa zima. Wajibu huo unatimizwa kwa kushiriki mtaguso mkuu, ambako ni
haki ya maaskofu wote, kuchangia muundo mpya wa sinodi ya maaskofu, kushughulikia kwa hali na
mali misheni na majimbo yasiyo na mapadri au mali za kutosha, kuwaombea maaskofu wafungwa na
wanaodhulumiwa, kuchangia katika ofisi za Papa.
Pili, ni wajibu wa baadhi ya maaskofu kuchunga kwa jina la Bwana sehemu fulani ya taifa la Mungu
wakitimiza kazi za kufundisha, kutakasa na kuongoza kama wachungaji halisi, ingawa wanapaswa
kuheshimu mamlaka ya Papa, patriarki na askofu mkuu. Chini ya askofu wake jimbo ni Kanisa
maalumu ambamo Kanisa pekee linaishi na kutenda. Hati hii inaelekeza namna ya kutimiza wajibu huo
(pamoja na kutaka utungwe mwongozo maalumu ambao ufafanue zaidi), inaagiza mipaka ya majimbo
irekebishwe yasiwe makubwa mno wala madogo mno, na inaratibu uhusiano na maaskofu waandamizi
na wasaidizi, nafasi ya makamu na halmashauri za askofu, uhusiano na maparoko na mapadri
wengine. Suala lingine gumu linahusu watawa (kwa namna ya pekee walio mapadri), ambao
wamehimizwa waishi kweli kama viungo vya jimbo na kujihusisha na maendeleo yake ya Kiroho na ya
kitume kwa kushirikiana na askofu, mapadri na walei pamoja na watawa wengine. Pia maaskofu wazee
au wenye shida nyingine wanahimizwa kujiuzulu.
Tatu, maaskofu wanadaiwa wachangie ustawi wa Kanisa katika maeneo yao kupitia sinodi,
mitaguso ya kanda au ya nchi, mabaraza ya maaskofu, ushirikiano katika kanda, pia na maaskofu
waliopewa kazi tofauti na jimbo (k.mf. uchungaji wa askari wote wa nchi yao).

PERFECTAE CARITATIS

Siku hiyohiyo iliyotolewa hati juu ya maaskofu ilitolewa nyingine kuhusu kurekebisha upya maisha
ya kitawa, nayo pia msingi wake ni hati Lumen Gentium juu ya Kanisa ambamo watawa wana nafasi
yao (sura ya sita). Mtaguso ulitaja tu marekebisho makuu ya kufanywa, ukimuachia Papa atunge
sheria hapo baadaye. Hasa ulisisitiza hali mpya ya utawa inayotakiwa kutokana na mambo matano:
kushika Injili kama kanuni kuu, kufuata kiaminifu karama ya mwanzilishi na mapokeo bora ya shirika,
kujihusisha na maisha na malengo yote ya Kanisa, kupima hali na mazingira ya watu wa leo, kuweka
mbele maisha ya Kiroho kuliko mipango mingine. Ili kuzingatia hayo yote, sheria za watawa
zirekebishwe kwa kuwahusisha wanashirika wote.
Kabla ya kueleza aina mbalimbali za utawa, hati inasisitiza mambo kadhaa yaliyo sawa kwa zote:
kushika mashauri ya Kiinjili, kujikatalia malimwengu, kuwekwa wakfu kwa Mungu juu ya msingi wa
Page 17 of 21


18
ubatizo, kulitumikia Kanisa, kutekeleza maadili, kumfuata Kristo kwa bidii kama jambo pekee la
lazima, kuunganisha sala hasa na moyo wa kitume. Nafasi ya kwanza ni ya maisha ya Kiroho yaliyo
chemchemi ya upendo unaohuisha utekelezaji wa mashauri ya Kiinjili. Watawa katika kulisha maisha
ya sala wazingatie kila siku Maandiko matakatifu halafu liturujia.
Katika kutofautisha aina za utawa, yanatajwa kwanza mashirika yanayoshughulikia sala tu katika
upweke na kimya; halafu mashirika yale mengi yaliyoanzishwa yatimize huduma maalumu kwa niaba
ya Kanisa na kama sehemu ya maisha yao ya kitawa; mwishoni mashirika yanayotakiwa kuunganisha
kiaminifu ratiba ya sala na taratibu nyingine za kijumuia pamoja na utume fulani.
Halafu hati inatamka maisha ya mabradha na masista ni muhimu yalivyo yasihitaji kuongezewa
daraja takatifu. Vilevile inasisitiza sura ya mashirika ya kilimwengu yanayopaswa kutafuta utakatifu
kwa kuishi katika mazingira ya watu wa kawaida: kwa ajili hiyo yanahitajika malezi bora.
Baadaye hati inarudi kufafanua mambo yanayowahusu watawa wote, hasa mashauri makuu matatu
ya Kiinjili, ikitanguliza useja kwa kuwa ndio msingi hasa wa kubainisha waliowekwa wakfu kwa Mungu
na kwa ufalme wake kwa namna ya pekee. Hati inaonyesha ubora wa useja na njia za kuushika
sawasawa baada ya jaribio la kutosha. Halafu inasisitiza ufukara kama ushahidi unaothaminiwa sana
siku hizi: basi, usiwe wa kiroho au wa binafsi tu, bali uonekane wazi katika maisha ya jumuia pia.
Kuhusu utiifu umesisitizwa ukuu wa sadaka hiyo ambayo mtawa anaungana kwa hakika na matakwa
ya Mungu kwa mfano wa Yesu. Pamoja na hayo ajitahidi kuwajibika chini ya viongozi akitoa mchango
wake kama mtu aliyekomaa. Pia mikutano na halmashauri vishiriki katika uongozi. Upande wao
viongozi wasitawale kwa mabavu bali waonyeshe upendo wa Mungu kwa mtawa, wakimheshimu na
kumsikiliza na kumuachia nafasi ingawa wana haki na wajibu wa kumuagiza la kufanya.
Sifa nyingine ya mashirika ya kitawa ni maisha ya pamoja ambayo yamesisitizwa upya kwa kutia
maanani misingi yake na utekelezaji wa upendo kamili katika ushirika wa kidugu. Kwa lengo hilo
matabaka kati ya masista yafutwe; mabradha washirikishwe zaidi katika maisha ya jumuia, hata kuna
kibali cha kuleta usawa kati ya wanashirika wakleri na walei.
Ili kulinda utawa toka zamani unatumika ugo, ambao kwa baadhi ya watawa wa kike unafuata
sheria za Papa. Hati hii inadai hizo zirekebishwe, halafu zisibane masista wanaofanya utume. Kinga
nyingine ya watawa wote ni vazi maalumu. Kwa mara ya kwanza katika historia mtaguso uliongelea
suala hilo na kulitia maanani kama alama ya kuwekwa wakfu, pamoja na kuagiza baadhi zibadilishwe.
Malezi yanasisitizwa sana kama msingi wa urekebisho, hivyo watawa wasitumwe kufanya shughuli
mara baada ya unovisi, bali wazidi kuundwa katika nyumba maalumu. Halafu malezi yaendelee maisha
yote kwa ushirikiano wa watawa na viongozi wao, ambao wajitahidi hasa kuandaa walezi wa kufaa.
Zinafuata taratibu za kuunda mashirika mapya, halafu za kueneza aina mbalimbali za utawa katika
Makanisa machanga kwa kuzingatia utambuzi na utamadunisho. Mashirika yaendelee kutimiza shughuli
zake maalumu kulingana na karama na nyakati pamoja na kustawisha moyo wa kimisionari. Yale
yasiyostawi yakatazwe yasipokee tena wanovisi au yaunganishwe na mengine yanayofanana nayo.
Tofauti na muungano, mtaguso umependekeza pia shirikisho la monasteri au mashirika ya familia moja
ya kiroho, vyama vya mashirika yenye kazi ileile, mabaraza ya wakuu wa mashirika yote ya nchi au
jimbo fulani ili kurahisisha ushirikiano kati ya watawa, tena kati yao na maaskofu.
Suala la mwisho ni namna ya kupata miito ya kitawa: hiyo ni kazi ya Kanisa lote, kuanzia mapadri,
wazazi na walezi. Mashirika yenyewe yanaweza kujitafutia miito kwa kufuata taratibu za Kanisa, lakini
njia bora ni kutoa mfano mzuri. Hatimaye watawa wote wanahimizwa kuitikia upya wito wao.

OPTATAM TOTIUS

Siku hiyohiyo ilitolewa hati nyingine tena inayohusu malezi ya kipadri: hayo yanatiwa maanani sana
kwa kuwa urekebisho unaotumainiwa wa Kanisa lote unategemea kwa kiasi kikubwa upadri ukitimizwa
kwa roho ya Kristo. Kuhusu jambo hilo mtaguso ulikusudia kulinganisha mang’amuzi ya karne zilizopita
na mahitaji mapya. Kwa kuwa malezi yanapaswa kuwa tofauti kwa kila mtu na kila aina ya watu, basi
maagizo ya hati hii yanayolenga kulinda umoja wa upadri, yatekelezwe kwa namna tofauti kadiri ya
mazingira, madhehebu na aina ya upadri (watawa, wanajimbo waseja na wenye ndoa).
Kwanza jumuia nzima inapaswa kuwajibika kwa malezi ya vijana na ustawi wa miito hasa kwa njia
ya sala. Wakurugenzi wa miito wasishindanie vijana, bali tujifunze wote kuwa na mtazamo wa Kikanisa
na wa kimataifa. Njia ya kawaida ya kuotesha mbegu za miito ni seminari ndogo. Hizo si za lazima,
kinyume na seminari kuu ambapo malezi yote yanalenga upadri moja kwa moja. Walezi wachaguliwe
kati ya mapadri bora, kwa kuwa malezi yanawategemea hasa wao. Waseminari waendelee
kuchambuliwa kwa imani ya kwamba Mungu hatakubali Kanisa likose wahudumu ikiwa wasiofaa
wanaelekezwa kwingine. Namba nyingine zinahusu malezi ya Kiroho, upendo kwa Kanisa, malezi ya
kijinsia, ukomavu wa kibinadamu na uwezekano wa kurekebisha sheria. Yanafuata maagizo kuhusu
masomo yenyewe, ambayo moyo wake uwe Biblia, na masomo ya juu. Pia inasisitizwa kuwa masomo
na malezi hayo yote yanalenga uchungaji katika nyanja zote.
Page 18 of 21


19

APOSTOLICAM ACTUOSITATEM

Mtaguso uliwaongelea walei katika hati mbalimbali ukionyesha nafasi yao katika maisha ya Kanisa
(liturujia, upashanaji habari, ekumeni n.k.). Hata hivyo uliona haja ya kuwaandikia hati maalumu
iwaongoze hasa katika utume ili watimize wajibu wao kwa wokovu wa ulimwengu. Karibu waamini
wote ni walei, na ndio wanaoshirikiana zaidi na watu wowote katika yote: hivyo wasipotoa mchango
wao, utume wa Kanisa utakuwa mlemavu, hasa siku hizi. Si kwamba wanapaswa kufanya utume
kutokana na upungufu wa mapadri na watawa, bali kutokana na wito walioupata katika ubatizo na
kipaimara.
Sura ya kwanza inaeleza wito huo katika Kanisa na roho itakayowezesha kuutimiza kitakatifu, kwa
sababu ni tofauti na ule wa mapadri na watawa, hivyo maisha ya Kiroho pia yanahitaji kuwa tofauti.
Sura ya pili inaeleza malengo makuu ya utume wa walei, kwamba si tu kueneza ujumbe wa Kristo,
bali pia kuratibu malimwengu yafuate matakwa ya Mungu, kutimiza matendo ya huruma na
kushuhudia upendo.
Sura ya tatu inafafanua zaidi nafasi mbalimbali za utume wao: jumuia za Kikanisa, familia, vijana,
jamii, taratibu za kitaifa na za kimataifa.
Sura ya nne inaeleza namna za kutimiza utume, kuanzia ule wa mtu mmojammoja hadi ule wa
pamoja katika vyama mbalimbali, ambavyo walei wana haki ya kujiundia, na katika miundo
iliyoanzishwa na wachungaji wao.
Sura ya tano inaeleza utaratibu wa kufuatwa ili utume usifanyike kwa wivu na ushindani bali kwa
upendo na ushirikiano, kwanza na maaskofu, mapadri na wahudumu wengine mpaka na Wakristo wa
madhehebu tofauti na wasio Wakristo. Kwa ajili hiyo iwepo halmashauri katika ngazi zote.
Hatimaye sura ya sita inasisitiza haja ya malezi bora kuanzia utoto na ujana na katika nyanja zote
zinazohusu utu na Ukristo. Halafu yawepo malezi maalumu kwa ajili ya shughuli za pekee.

AD GENTES

Siku ya mwisho kabla ya kufunga mtaguso zilitolewa bado hati tatu, mojawapo kuhusu umisionari
wa Kanisa, yaani aina ile ya utume inayowaelekea wasio Wakristo, ambao ndio wengi zaidi (thuluthi
mbili za watu wote). Kazi hiyo ni tofauti na uchungaji (unaowaelekea Wakatoliki) na ekumeni
(inayowalenga Wakristo wengine).
Sura ya kwanza inafafanua misingi ya umisionari: hasa upendo wa Baba uliomfanya amtume
Mwana halafu kwa jina lake amtume Roho Mtakatifu kwa Kanisa lililotumwa na Yesu kuendeleza kazi
yake. Basi, umisionari unatokana moja kwa moja na umbile la Kanisa, na kudaiwa na azimio la Mungu
la kutaka watu wote waokoke na kujua ukweli. Umisionari unawakusanya pia watu katika umoja na
kuharakisha ujio wa ufalme wa Mungu.
Sura ya pili inaeleza utendaji wenyewe kuanzia ushuhuda wa maisha ya Kikristo na wa matendo
yaliyojaa upendo. Kwa ajili hiyo waamini wahusiane na kujadiliana vema na watu wengine. Juu ya
msingi huo inaweza kufanyika kazi ya kuwahubiria Injili na kuwakusanya katika taifa la Mungu. Hati hii
inakataza katakata wasilazimishwe wala kuvutwa kwa udanganyifu wakubali imani, kama vile
inavyodai wasizuiwe kufuata imani. Baada ya kuchunguza na kunyosha sababu za uongofu wao,
waliojaliwa mwanzo wa imani wapokewe kwa ibada maalumu katika ukatekumeni ambao ufuate
maagizo mbalimbali ya mtaguso. Kisha kubatizwa waishi kijumuia kama familia ya Mungu, ambayo itie
kweli mizizi katika makabila yao, hasa kwa njia ya walei. Pamoja nao Kanisa, likilenga mara
kujitegemea iwezekanavyo katika miundo yote, linahitaji zaidi na zaidi wahudumu kutoka makabila
hayo mpaka liundwe jimbo lenye askofu, mapadri, mashemasi, watawa na makatekista wenyeji.
Sura ya tatu inajadili Makanisa maalumu ikionyesha jinsi yale machanga yanavyoendelea na
kukomaa hata yakaanza kuwatuma mapadri, watawa na walei walio tayari kwenda kwa wasio
Wakristo, ndani ya jimbo na nje pia. Hivyo Kanisa lililokomaa katika mazingira yake linashirikisha
utajiri wa nchi husika, badala ya kuishia kukidhi mahitaji yake tu.
Sura ya nne inazungumzia wamisionari wenyewe, malezi yao na maisha ya Kiroho yanayopaswa
kulingana na wito wao maalumu. Ili kurahisisha malezi hayo na kazi hiyo Mungu alitokeza mashirika
yenye umisionari kama lengo kuu.
Sura ya tano inatoa maagizo ili umisionari uwe na umoja na kufanikiwa. Kimataifa Papa aratibu
umisionari kwa njia ya idara ya uenezaji imani, isipokuwa Makanisa ya mashariki yanafuata idara yao.
Vilevile kijimbo na kitaifa kuwe na miundo na ushirikiano kati ya mashirika.
Sura ya sita inapanua mtazamo kwa kuonyesha umisionari unavyohusu Kanisa lote kama wajibu
wake mkuu. Kwa hiyo ni lazima kila mwamini ajirekebishe na kuchangia wokovu wa wasio Wakristo.
Vilevile kila jumuia iwashughulikie walio mbali kwa bidii ileile inayowashughulikia walio jirani. Kwa
namna ya pekee wanapaswa kuwajibika maaskofu kama waandamizi wa mitume waliowekwa wakfu
kwa wokovu wa ulimwengu mzima. Baada yao mapadri waeneze moyo wa kimisionari ili miito ya
namna hiyo ipatikane na michango ifanikiwe. Tena mashirika yote ya kitawa, yawe ya sala tu au ya
utume, yafikirie upya yanavyowajibika katika umisionari. Hatimaye walei pia wana nafasi kubwa katika
kazi hiyo nchini kwao na kwenye misheni za mbali.
Page 19 of 21


20

PRESBYTERORUM ORDINIS

Hati hii pia ilitolewa siku ya mwisho kabla ya kufunga mtaguso ili kufafanua tena mambo kadhaa
yaliyokwishaelezwa na hati nyingine.
Sura ya kwanza inahusu upadri katika utume wa Kanisa, jinsi unavyounganisha mapadri na
maaskofu kwa ajili ya taifa la Mungu.
Sura ya pili inaeleza kwanza kazi tatu za mapadri, yaani kufundisha, kutakasa na kuongoza. Halafu
inasisitiza uhusiano wao na askofu, kati yao, tena na walei. Mwishowe inafikiria la kufanya ili kuwe na
mapadri wa kutosha: hiyo haitegemei tu bidii kwa ajili ya miito, bali pia ugawaji mzuri wa watenda kazi
katika shamba la Bwana.
Sura ya tatu inaingia zaidi katika maisha yao ikisisitiza wanavyopaswa kwa namna ya pekee
kulenga utakatifu, hasa kwa kutekeleza vema huduma zao na kuziunganisha katika kutimiza matakwa
ya Baba kama Yesu alivyofanya. Kati ya maadili wanayoyahitaji, hati inaeleza hasa mashauri ya Kiinjili
ya utiifu, useja na ufukara ambayo kwao yanalenga ubora wa huduma za kipadri (tofauti na watawa
wanaoyashika hasa ili kujipatia utakatifu). Ndiyo sababu kwa mapadri la kwanza ni utiifu, kumbe useja
si wa lazima (tunavyoona katika Kanisa la mwanzoni na katika Makanisa ya mashariki mpaka leo).
Baada ya hapo hati inakabili suala la kuwasaidia kwa namna mbalimbali: kwanza katika maisha ya
Kiroho, halafu kuhusu elimu hasa ya kidini, lakini pia kuhusu malipo ya haki na bima wasije
wakahangaika. Mwishoni mapadri wanatiwa moyo katika magumu yanayowakabili siku hizi, kwa
kukumbushwa kinachojulikana kwa imani tu, kwamba Mungu na Kanisa wapo pamoja nao.

GRAVISSIMUM EDUCATIONIS

Katika tamko hilo la kwanza mtaguso ulizingatia umuhimu wa malezi kwa mtu binafsi, kwa jumuia
zake, kwa nchi yake na kwa Kanisa lenyewe. Watu wa leo wanaelewa zaidi umuhimu huo kwa watoto,
vijana na hata watu wazima; ndiyo maana wanafanya mipango mingi wakitumia pia njia mpya
zilizoletwa na maendeleo. Kanisa linataka kuchangia juhudi hizo kufuatana na wajibu wake kwa watu
wote na kwa mtu mzima (mwili na roho).
Hati hii inasisitiza haki ya kila mtu ya kupata malezi ya kumfaa; vilevile waamini wote wana haki ya
kupata malezi ya Kikristo, hasa vijana, tumaini la Kanisa. Wazazi ndio walezi wakuu kwa watoto wao:
wasipoutimiza wajibu huo mkubwa, si rahisi kujaza pengo hilo. Familia isaidiwe na jamii na Kanisa kwa
njia mbalimbali, hasa shule: walimu waione kazi yao kuwa wito. Ni juu ya wazazi kuchagua aina ya
shule inayohakikisha watoto wao walelewe wanavyopenda wazazi wenyewe. Serikali haina haki ya
kulazimisha wote kupata malezi ya aina moja, bali inapaswa kusaidia shule huru za wazazi na za kidini.
Kanisa liwashughulikie Wakristo wanaosomea shule zozote, lakini lijitahidi kuwaanzishia shule
katoliki likiwahimiza wazazi kuwaandikisha huko watoto wao. Katika shule hizo elimudunia itolewe
katika mazingira ya imani ili Mkatoliki alelewe bila mgawanyiko wa ndani, ingawa wanafunzi wengine
pia wanaruhusiwa kupokewa. Shule katoliki zinaweza kuwa za namna mbalimbali na za ngazi zote,
kuanzia za chekechea hadi vyuo vikuu, pamoja na vyuo vya kufundishia dini tu. Kati ya shule hizo zote
ushirikiano ni muhimu.

NOSTRA AETATE

Kutokana na mchanganyiko wa watu, ambao siku hizi unaongezeka mahali pengi, mtaguso uliona
haja ya kutoa tamko juu ya uhusiano na dini nyingine ili kujenga umoja kadiri ya mpango wa Mungu.
Tamko hilo linasema kwanza juu ya dini za kimila, halafu juu ya zile zilizoendelea pamoja na elimu
(k.mf. Ubaniani na Ubudha): Kanisa linaheshimu dini hizo, ambazo ni tofauti sana na ya kwetu, ila
linazidi kuwatangazia wote kuwa Yesu ndiye njia, ukweli na uzima.
Katika nafasi ya pekee Uislamu unasifiwa kwa tunu zake nyingi. Mtaguso ukizingatia magomvi ya
zamani kati ya Wakristo na Waislamu umewahimiza wote kusahau yaliyopita ili kuelewana na
kushirikiana.
Mwishoni tamko linasifu Israeli likihimiza wote kufahamiana na Wayahudi na kuacha kuwalaumu
kwa makosa wasiyonayo. Kanisa linalaani dhuluma yoyote dhidi yao, ambao toka zamani wameteswa
mno hata na Wakristo na kwa visingizio vya Kiinjili. Kumbe bado ni wapenzi wa Mungu, nasi tunalishwa
na utomvu wa mizizi yao.
Basi ni juu yetu kuondoa ubaguzi wowote na kujenga udugu ili tuwe kweli wana wa Mungu.

DIGNITATIS HUMANAE

Tamko hilo la mwisho lilisababisha mijadala mikali wakati wa mtaguso na baada yake hata
likachangia kwa kiasi kikubwa farakano la askofu Lefebvre. Sababu ni kwamba linasisitiza haki ya
binadamu ya kufuata ukweli wa kidini kadiri alivyoujua, wakati mafundisho ya zamani yalikuwa
yakisisitiza kuwa imani ya Kikristo ni ya lazima kwa wokovu. Lakini masisitizo hayo hayapingani, kwa
maana ni wajibu wa kila mtu kuutafuta ukweli na kuufuata, ila hatuwezi kumlazimisha asiyejaliwa bado
imani au mwanga wa kutosha, bali tunapaswa kuendelea kumtangaza Yesu kwa wokovu wa watu.
Page 20 of 21


21
Kinyume cha baadhi ya matendo ya Wakristo wa zamani, Kanisa linaamini dini yetu inapaswa
kuenea kwa nguvu ya ukweli wake, si kwa upanga, kwa kuwa Mungu mwenyewe anamheshimu
binadamu na hiari yake. Mfano bora ni ule wa Kristo na wa mitume wake.
Basi, kila mtu na kila serikali waheshimu uhuru wa kufuata dini yoyote. Haki hiyo inahusu mtu
binafsi na makundi pia.

MTAKATIFU FRANSISKO NA MTAGUSO

Mzee wetu Fransisko anasifika kwa ukatoliki wake: alishikamana kabisa na Kanisa akiwatii viongozi
wake na kuwa rafiki yao. Tangu mwanzo alitaka kuweka utawa wake chini ya Mama Kanisa Takatifu la
Roma akakubaliwa kwa moyo. Kinyume cha uzushi mwingi wa wakati wake, karama ya Fransisko
ilionyesha wazi kuwa Injili imekabidhiwa kwa Kanisa, hivyo ishikwe kikamilifu ndani ya Kanisa na kwa
msaada wake.
Tukiangalia zaidi uhusiano huo tunaona Fransisko alivyoingia kabisa katika juhudi za urekebisho wa
liturujia na maadili ambazo kilele chake ni Mtaguso IV wa Laterano (1215). Wengi wanadhani
mwenyewe aliuhudhuria akiwa mkuu wa utawa; kwa vyovyote alionekana kujua sana malengo na
maamuzi ya mtaguso huo, na kutaka kuyatekeleza pamoja na wafuasi wake na waamini wote.
Kwa mfano, barua zake zinahimiza kuheshimu ekaristi na yale yote yanayohusu liturujia: katika
kuziandika alitumia hata maneno ya hati za mtaguso na za Papa. Zaidi tena, Fransisko alipokea kwa
moyo mpango wa Inosenti III wa kufanya Kanisa lote (hasa wakleri) liongoke kwa kusulubisha mwili
na tamaa zake, likitumia ile tau inayoongelewa na Ezekieli 9 kuwa muhuri waliotiwa wateule wa Mungu
waliokubali msalaba katika maisha yao. Hivyo tau ikawa kwa Fransisko pia ishara ya toba aliyojitahidi
kuieneza kati ya waamini. Kwa kuungana kabisa na Msulubiwa na kuongozwa na Roho Mtakatifu katika
yote, akawa chombo cha kurekebishia Kanisa si kwa kulilaumu wala kwa kulipinga, bali kwa kuishi
kitakatifu.
Kanisa linajikuta leo katika hali inayofanana na ile ya zamani za Fransisko na linahitaji watu ambao
wamefanywa wapya kwa kushiriki mateso ya Kristo, na ambao Roho aweze kuwatumia bila pingamizi
kwa ujenzi wa ufalme wa Mungu. Mtaguso II wa Vatikano umepanga kwa upana wote kazi ya
kutengeneza upya maisha ya Kikristo, lakini kazi hiyo haiwezi kufanyika bila mwanga na nguvu ya
Roho Mtakatifu, naye anafanya kazi hasa katika watu waliokubali kujazwa naye hata kuwashirikisha
ndugu zao.
Basi, mfano wa Fransisko unawahimiza Wakristo washikamane na Kanisa kwa nguvu zao zote;
ndani yake mfumo au muundo wowote usikubali kuwa na mpango wake wenyewe tu, bali utumie kwa
unyenyekevu karama yake katika kutimiza mpango uliofanyika katika mtaguso kwa ushirikiano wa
Roho na maaskofu wote. La sivyo miongozo na maagizo yake bora yatabaki maandishi matupu yasizae
matunda yote yaliyotarajiwa. Hasa Kanisa linatazamia wafuasi wote wa Fransisko watatoa mchango wa
utakatifu wao ambao kwa namna fulani umfufue kwa ulimwengu wa leo.
Page 21 of 21

21 of 21


Rejea
ttps://drive.google.com/file/d/0B9npUSHEVehzanBPYXBrUEpfUGM/view

Displaying Mitaguso Mikuu.pdf.
Comments